BUJUMBURA, BURUNDI

KUENDELEA kuwepo kwa Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Burundi kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi, kumeendelea kuzua mgawanyiko nchini humo.

Serikali ya Burundi inaishtumu Tume hiyo kuongezewa muda, huku wanasiasa wa upinzani wakiunga mkono kuendelea kuwepo nchini Burundi kwa wajumbe hao wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujubu wa balozi wa Burundi katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Rénovat Tabu, azimio la kurefusha muhula wa tume hiyo ya haki za binadamu Burundi ni njama za Umoja wa Ulaya tangu mzozo wa mwaka 2015.

Alisema ni dhahiri kuwa Umoja wa Ulaya uliunga mkono kwa hali na mali makundi ya waandamanaji walioshirikiana na wanasiasa pamoja na askari kwa kujaribu kuipindua serekali tarehe 13 Mei mwaka 2015.

“Kamwe Burundi haitoshirikiana na tume hiyo. Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, matatizo ya Burundi si ya haki za binadamu, bali ni ajenda ya kisiasa inaodhamiria kupasishwa kwenye Baraza la Haki za Binadamu”, alisema balozi huyo.

Kwa upande wake Phéneas Nigaba, msemaji wa chama cha Frodebu, cha upinzani nchini Burundi, aliiomba serikali iwaruhusu wajumbe wa tume hio ya haki za binadamu kuingia nchini Burundi.

“Burundi haiwezi kusema kila mara kuwa tume hio sio lazima, wakati ilipoundwa, chanzo ni machafuko. Je haki za binadamu zinaheshimishwa?”, alisema kiongozi huyo.

Azimio la kuunda Tume hio ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi kuhusu haki za binadamu nchini Burundi lilipitishwa Septemba 30 mwaka  2016, na wajumbe wake bado hawajaruhusiwa kuingia nchini Burundi.