NA KIJA ELIAS, MOSHI

CHAMA Cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro (CCM), kimempongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli, kwa kuapa kuzilinda  rasilimali za  taifa.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mstaafu wa UV-CCM Mkoa wa Kilimanjaro Mwalim Yasin Lema, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya matembezi ya amani na mshikamano katika kumuenzi hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake Rais Dk. Magufuli, amejaribu kupitia kwenye nyayo za Mwalimu Nyerere, ikiwemo usimamizi wa rasilimali za taifa, licha ya kwamba wapo baadhi ya watu wameibuka na kuanza kupinga jitihada hizo huku akiwataka Watanzania kuwapuuza.

“Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere, alifanya mambo makubwa katika nchi hii, yapo mambo ambayo alikuwa akiyasema kila mara wakati alipokuwa akizungumza kwenye hotuba zake, alisisitiza sana suala la mshikamano, kuondoa ubaguzi, mambo ya udini na mengine mengi,’alisema Lema.

Lema alisema Mwalimu Nyerere alikuwa na maono ya mbali, alijua wazi kwamba kuingia kwenye shughuli za uchimbaji wa madini bila kuwa na uelewa wa kutosha, ni hatari kubwa kwa taifa kwa sababu mwisho wa siku, watakaonufaika na rasilimali za madini, watakuwa ni wale wajanja wachache.

“Suala la maliasili za nchi yetu, haswa madini  mwalimu alikuwa na msimamo kwa kuwataka madini haya yasichimbwe, tungoje kwanza wenye nchi yao wakue, wasome waje wachimbe madini yao,”alifafanua.

Kwa upande wake Kaimu Katibu wa UV-CCM mkaoa wa Kilimanjaro Bulugu Magege, alisema umoja na uhuru ni tunu ya taifa iliyoachwa na hayati Mwalimu Nyerere na kwamba zinatakiwa kutunzwa kwa nguvu zote bila kujali tofauti zilizopo za kiitikadi.