TOKYO,JAPAN

UWANJA wa Ndege wa Narita jirani na Tokyo unapunguza ada za utuaji wa ndege uwanjani hapo kwa kuwa mashirika ya ndege yanapambana na janga la virusi vya corona.

Kampuni ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Narita ilisema inafuta ada za utuaji kwa safari za ndani za abiria, na kupunguza ada kwa takribani asilimia 30 kwa safari za kimataifa.

Janga la corona limeiathiri vikali sekta ya usafiri wa anga. Idadi ya wasafiri wanaotumia uwanja wa ndege wa Narita ilipungua na kufikia rikodi ya chini kabisa ya wasafiri milioni 1.36 kati ya Aprili na Septemba mwaka huu.

Kampuni hiyo ilisema kuwa haitaongeza ada tena hadi pale idadi ya abiria itakapoanza kuongezeka tena.

Wizara ya Usafirishaji ilisema Narita ni uwanja wa ndege binafsi wa kwanza nchini Japani kupunguza ada za utuaji kufuatia janga la virusi vya corona.