NA HAJI NASSOR, PEMBA

NI majira ya saa 12:50 asubuhi, miale ya jua imeanza kuchomza kwa mbali, yakiangaza angaza, kwenye miti mirefu kama Miembe na Minazi.

Hapa nipo kijiji cha Mkungu, shehia ya Mkungu wilaya ya Mkoani Pemba, ni kilomita zaidi ya 25 kutoka mji wa Chake chake, ambao ndio kitovu cha kisiwa cha Pemba.

Eneo hili kwa usafiri wa gari ya abiria kutoka mjini Chake chake, ni mwendo wa dakika 45, ingawa kwa gari ya isiyokuwa ya abiria muda unaweza kuwa mdogo kwa kuwa haipiti na kusimamasimama.

Mkungu ambayo imepakana na vijiji vya Mahuduthi, Sipwese, Mitunda fumoni na barabara kuu itokayo Mtambile kwenda Kengeja, wakaazi wake wengi wao ni wakulima.

Kijiji hichi, kama vilivyo vijiji vyengine, wapo vijana wanaojihisi hawana kazi rasmi ya kufanya, na hivyo kila mmoja kufanya shughuli yake kipekee.

Wanaharakati wanaamini kuwa, kujikusanya pamoja na kuendesha shughuli maalum, ni mwendo wa njia ya mkato wa kufikia malengo waliyojiwekea.

Hilo vijana wa hapa Mkungu, walilikimbia mapema na wao walimua kujikusanya pamoja na kufikia 20, na wengi wao kwa hamu na uchu wa maendeleo, wanawake ni 15 na wanaume watano.

Kikundi hichi cha ‘Mola tuwezeshe’ kilanzishwa mwaka mmoja uliopita, baada ya kujitokeza kwa watendaji wa Chama cha Waandishi wa habari Tanzania -TAMWA-Ofisi ya Zanzibar, tena kisiwani Pemba, kutaka vijana wajiajiri.

Hapa, kwa vijana hawa wa Mkungu, na ujio wa TAMWA chini ya Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Zanzibar (WEZA III), imekuwa ni faraja kwao kwani yale matumaini ya kufikia maisha bora ndoto zao zitatimia muda si mrefu.

Mshika fedha wa ushirika huo, Nassra Mohamed Habib, anasema baada ya kufikiwa na WEZA III, na kupewa elimu ya ufugaji, walilazimika kukusanya nguvu zao, ili waanze kutafuta mifugo.

“Kwa kweli mradi huu umekuja sasa kutuamsha, maana kwanza, walitupa elimu ya ufugaji, na sisi baada ya kuipokea, kwa vile tuko wanachama 20, kila mmoja alilazimika kuleta kuku mmoja kwa kuanzia,’’anasema.

Huku Mshika fedha akiyasema hayo, Katibu wa ushirika huo Suleiman Massod Khalfan, alinivuta pembeni ni kunieleza kuwa, vijana hao wa kijiji chao, awali walishapigwa kimaisha.

Haya sasa, yamegeuka na kuwa ya ukweli, maana kupitia ufugaji huo na uwekaji wao hisa, wapo wanachama wameshakopa hadi shilingi 300,000 na kujinunulia hadi cherani.

Akizungumza na makala haya, Mwanachama wa ushirika huo, Faida Massoud Khalfan, yeye kwa sasa anajiamini wakati na saa yeyote, kukopa fedha kupitia ushirika wao na kuzirejeshwa kwa wakati.

“Kwa hakika wadsau wetu hawa wamekuja kutuonesha njia na sasa tumeshaanza kuifuata na matunda yapo, hivyo tumeshavunja makali ya umaskini”, anasimulia.

Anasema mradi huo ni mfano kwao, kwanza umewashawishi kuanzisha miradi, pili kuwapatia elimu ya ufugaji na sasa, wao vijana wa kijiji hicho wameshapiga hatua ya maendeleo.

“Elimu tuliyopewa na wataalamu kutoka TAMWA, sasa imetuwezesha walau kujua aina ya maradhi ya mifugo, mfano ndui yanayowasibu kuku na ikitokeza vipi tufanye”, anasema.

Hivyo ushirika huo pamoja na ufugaji wa kuku wa kienyeji na kuanzisha mpango wa kuweka na kukopa, na sasa wastani wa shilingi mioni 4, zimo mikononi mwa wanachama wao baada ya kukopeshana.

Huu ni ushirika mmoja tu, lakini TAMWA inavisimamia vikudni 48 kisiwani Pemba, ambavyo vinakusanya vijana wa kike na kiume wafikao 960 kwa wastani wa vijana 20 kila kimoja.

Maana, hata ushirika wa ‘mtaji wa maskini’ kijiji cha Mahuduthi ambao unao una wanachama 20, sasa baada ya ushajihishwaji, wameshalima kilimo cha tungule na mchicha.

Mwanachama Said Khamis Suleiman, anasema hivi sasa maisha yao yamebadilika sana baada ya kupata taaluma na sasa kuanza kuzalisha vitu mbalimbali kama ufugaji wa kuku.

Anasema, sasa kwenye eneo hilo pekee wanaweza kujiingizia wastani wa shilingi 250,000 kwa mwezi na hasa kama kilimo chao cha tungule, bamia, mriba, bilingani hakikukumbwa na changamoto za ukosefu wa maji na kuvamiwa na wadudu.

Haya yakiwasogelea vijana kufikia pato lao la juu zaidi, sasa ushirika huu, umeshavuna majani ya mti aina ya mchai chai watsani kilo nne na kuukausha na wakati wowote kuanzia sasa, watakuwa wazalishaji pekee kwa eneo hilo kwa majani ya chai.

Nae mwanachama Safia Othman Juma, alisema kama mpango wa kuzalisha majani ya chai kupitia majani ya mchai chai, hapo umaskini kwao utakuwa ndoto.

“TAMWA ilikuja kutuzindua, maana elimu waliyoputa na sasa tuna hadi visanduku na kilimo mchanganyiko, si haba maisha magumu yamepungua makali yake,’’anaeleza.

Mwanachama mwengine wa ushirika huo, Moza Mohamed Salum anasema, hata ufugaji nao sasa wanataka kuuendeleza, baada ya hapo awali kukumbwa na changamoto ya magonjwa.

“Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi Zanzibar kama ungekuja miaka 10 nyuma hapa kijijini kwetu, sasa wanawake na vijana wengekuwa wako imara ya kuziendesha familia zao,” anasema.

Ndani ya ushirika huu, wapo wanachama ambao walikopa fedha kati ya shilingi 200,000 hadi shilingi 300,000 kwa kwa mtu mmoja nakujiendeleza kimaisha.

Kwa mfano, kijana Mohamed Khamis Salim alikopa shilingi 500,000 na kuziingiza kweye uendelevu wa ujenzi wa nyumba yake ya kisasa na tayari ameshahamia.

Anasema, kama si kuwepo kwa ushirika huo, basi suala la kuanzisha au kujenga, kwake lingekuwa ndoto, lakini sasa anatembea kifua mbele.

Nae Mratibu wa miradi hii Pemba, Asha Mussa Omar, kutoka TAMWA- Pemba anasema miradi ya wadau hao wa masuala ya wanawake imekuja kwa kasi mpya na ya  aina yake, kuwawezesha kundi la vijana na wanawake.

Anasema kupitia mradi huo, vijana wanaweza kukomboka na kupunguza fmaombi ya ajira kwenye  ofisi za serikali, kwa kusaka ajira.

“Katika hili, kama ilivyo miradi mengine, unataka kuona vijana wanajiajiri kupitia rasilimali zilizopo katika maeneo yao,” anafafanua. 

Anasema, kuwa na maisha mazuri na bora wala sio lazima kuajiriwa serikalini au kwenye makampuni makubwa kama ndoto za baadhi ya vijana zilivyo, bali matumizi sahihi ya rasimali yanaweza kuwakomboa.

“Ndio maana wapo waliobuni miradi kama ya upandaji wa vitunguu, tangawizi, manjano, mchicha, ufugaji kuku, bamia, utengenezaji sabuni na sisi tuko nao bega kwa hadi wang’are,’’anasema.

Hata hivyo, aliziomba taasisi nyingine, ambazo zinatetea haki za vijana, wanawake na watoto kuvikimbilia vikundi hivi na kuvipa mikopo yenye masharti nafuu au mitaji mikubwa ili waweze kuendesha maisha yao kwa kufanya miradi mbalimbali.

“Wakati mwengine vijana wanaanzisha miradi, lakini wanapohitaji mikopo kwenye taasisi husika, hukumbana na masharti magumu, lazima hili lifikiriwe upya,’’anasema.

Moja ya kijiji kilichofaidika na mradi huo ni Sipwese shehia ya Mkungu wilaya ya Mkoani, ambako vijana 20 waliounga nguvu zao pomoja na kuanzisha ushirika unaoitwa ‘Kheir Liwe’.

Vijana hawa ambao nao wanakiri kuwa, kufumbuliwa macho na TAMWA, sasa maendeleo makubwa kupitia shughuli yao ya kilimo, wanaifikiria.

Kwa idadi hii ya vijana 20 waliopo kijiji cha Sipwese hapo awali, sasa wamefikia vijana 960 kutoka kwenye vikundi 48 kisiwani Pemba.

Nae Asha Khamis Nassor, ambae ndie Mwenyekiti wao, anasema kama kilimo chao cha mchicha, bilingani, bamia na mriba wakivuna kwa pamoja, watajizolea mapeni mengi.

“Sisi kama tutavuna kwa umoja, basi hadi shilingi 300,000 ndio haki zetu na hapo itakuwa tumeshapiga hatua, maana kabla ya ujio wa mradi huu hatukuweza kuwa

“Kwenye faida, wapo wanachama akiwemo Hafsa Zubeir Haji aliwahi kukopa shilingi 200,000 na kununua nguo na kuuza na kujiingiza faida, kati ya shilingi 80,000 hadi shilingi 100,000, anasema.

Nae mwanachama Mmanga Abdalla Omar, alikopa shilingi 200,000 kupitia ushirika wao wa ‘Kher liwe’ na kununua shamba la muhogo.

“Mimi, baada ya kununua sehemu ya shamba hilo, niliusarifu kwa kuufanya makwaru, na si haba nilipata faida ya shilingi 100,000 baada ya kutoa hasara zangu zote,’’ananisimulia.

Ushirika huu, kama ilivyo kwa vyengine, wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa mashine za kusukumia maji, kwa ajili ya vipando vyao.