KABUL,AFGHANISTAN

KURUGENZI ya kitaifa ya usalama nchini Afghanistan NDS imesema kuwa vikosi vya usalama nchini humo vimemuuwa kiongozi mmoja mkuu wa kundi la al-Qaeda Abu Muhsin al-Masri aliyekuwa katika orodha ya shirika la upelelezi la FBI ya wanaosakwa zaidi kwa ugaidi.

Al-Masri alikuwa ameshitakiwa nchini Marekani kwa kutoa ufadhili wa bidhaa na raslimali kwa shirika moja la kigeni linalohusika na ugaidi na pia kwa njama ya kuwauwa raia wa Marekani.

NDS ilisema kuwa Al-Masri anayeaminika kuwa wa pili mwenye ushawishi zaidi katika kundi hilo la al-Qaeda, aliuawa wakati wa operesheni maalumu katika mkoa wa Ghazni Mashariki mwa Afghanistan na kuongeza kuwa alikuwa kiongozi mkuu wa kundi hilo katika eneo la bara Hindi.

Mwezi uliopita, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema kuwa wanachama chini ya 200 wa kundi hilo walibakia nchini Afghanistan.