NA LAILA KEIS

TIMU ya soka ya Jang’ombe Boys kwa mara ya kwanza imefanya uchaguzi wa kidemokrasia kwa kuchagua viongozi wapya.

Kauli hiyo imetolewa na rais wa timu  hiyo Ali Othman Ali (Kibichwa), wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika uchaguzi wa kuwachagua viongozi wapya hivi karibuni.

 Alisema uchaguzi huo ulioshirikisha wanachama 108, ambao walimchagua Ali Othman Ali kuwa rais, kwa kupata kura 99, na Ali Mohammed Ali kuwa  Makamu wa rais kwa kupata kura  108.

Kibichwa alisema wanachama hawajakosea kumchangua na atahakikisha anaiongoza vyema, ambapo malengo yake ya kwanza kuirejesha ligi kuu Zanzibar msimu ujao baada ya kushuka daraja msimu uliopita.

Nae Makamu wa rais wa timu hiyo, Ali Mohammed Ali alisema raha ya uongozi katika klabu, ni pale wanachama wanapochagua viongozi wenyewe, jambo ambalo  huondosha migogoro na kuweka  heshima katika timu.

Aidha alisema timu yao inachangamoto nyingi ikiwemo baadhi ya wanachama kujenga tabia mbaya ya kutoa matusi wakati  wa michezo yao viwanjani.

Hivyo alisema uongozi uliochaguliwa una mikakati ya kulidhibiti tatizo hilo, huku wakishirikiana na taasisi mbali mbali ili kutoa elimu kwa wanachama wao.

Nae mmoja ya wanachama wa klabu hiyo, Kassim Jecha, alisema, wana imani na viongozi hao, kwani wamewachagua kutokana na kuona juhudi zao za kuleta maendeleo ya timu, hivyo wataendelea kuwaunga mkono.

Tokea kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1998, ni mara ya kwanza kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.