NA ZAINAB ATUPAE

VYAMA vya siasa nchini vimeshauriwa kufuata muongozo na taratibu zote zinazotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo ipo kihalali katika kufanya kazi zake.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mwenezi wa tawi la CCM la Kiponda, Mohamed Saleh Momhamed, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko Ofisi za shirika la gazeti hili ziliopo Maisara Unguja.

Alisema Tume ya Uchaguzi ipo kihalali katika kufanya kazi zake, hivyo hakuna budi kwa vyama hivyo kufuata miongozo ambayo imewekwa katika suala zima la uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 na baada ya uchaguzi huo.

Alisema endapo vyama hivyo vitafuata taratibu zilizowekwa na Tume basi hakuna baya ambalo linaweza kutokea kwenye uchaguzi huo na kila chama kitaridhika na matokeo atakayo yapata.

Aidha alitoa wito kwa vijana,wazee wakiwemo wanaume na wanawake, kujiepusha na vurugu za aina yoyote katika kipindi cha uchaguzi.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa kwenye mikutano yao wanahubiri maneno ya uchochezi ambayo yanalengo la kuchafua amani ya nchi.

Alisema ni vyema viongozi wanapokuwa kwenye kampeni zao kuhubiri sera ambazo zitaleta mvuto kwa wananchi wake, na sio kuleta mambo ya uchochezi kama wanavyofanya baadhi ya vyama vyengine.

 “Ushindani sio ugomvi ni maneno mazuri ambayo yanamjenga mwananchi kuvutiwa na sera za mgombea Fulani na sio maneno ya uchochozi,”alisema.

“Mungu atujaalie tufanye uchaguzi wa salama na amaani katika nchi yetu ,kwani baada ya uchaguzi kuna maisha ya baadae,”alisema.