NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali amesema Chama Cha Mapinduzi kitapata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu, kutokana ushindani dhaifu wa vyama upinzani.

Dk. Bashiru alieleza hayo jana katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazunguzo kati yake na balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright.

Alisema CCM itashinda uchaguzi kwa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano na kiti cha Urais wa Zanzibar, kwani vyama vya upinzani mwaka huu ni dhaifu mno ikilinganishwa na mwaka 2015, ambapo baadhi ya vyama hivyo havina hata ilani.

Alisema ilani mpya mwaka 2020/2025 nayo imebeba miradi mingi ambayo inatekelezeka, hali ambayo ni kinyume na vyama vya upinzani ambavyo baadhi yao havina hata ilani na vyengine vimetunga ilani baada ya kuzindua kampeni za uchaguzi.

Dk. Bashiru alisisiza kuwa hakuna mgombea yoyote wa upinzani aliyekuwa tishio kwa wagombea wa urais wa CCM Tanzania na Zanzibar, ambapo vyama hivyo ni dhaifu na haviwezi hata kujieleza nini watawafanyia wananchi.

Alieleza baadhi ya vyama ni vipya kama ACT- Wazalendo ambacho kimezaliwa mwaka 2015, kilikuwa na mbunge mmoja kutoka Kigoma Mjini, na halmashauri mmoja na hakikukuwa na mwakilishi hata mmoja Zanzibar na wala wabunge.

Alisema Balozi wa Marekani anayewakilisha nchi yake Tanzania, alifika hapo alimueleza vipao mbele vyake ni pamoja na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizi na kueleza kuwa Marekani itaendelea kushirikiana katika huduma za afya kwa kukabiliana na maradhi ya kifua kikuu, UKIMWI na malaria.

Alieleza pia wanataka kushirikiana katika sekta ya uwekezaji, na biashara katika maeneo mbali mbali, ambapo Tanzania inavivutio vingi na kuhimiza suala la hifadhi ya mazingira ya wanyama pori, uhusiano katika sekta ya utalii, ambayo imekumbwa na changamoto ya ugonjwa wa corona.