NA MWANAJUMA MMANGA

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa za mafunzo ya amali zinazotolewa na taasisi mbalimbali ikiwa ndio njia pekee ya kuepuka changamoto ya ukosefu wa ajira.

Balozi Seif, aliyasema hayo jana katika mahafali ya vijana waliohitimu mafunzo ya ujuzi wa ufundi katika vyuo vya Amali kwa Unguja na Pemba kwa mwaka 2020 katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil.

Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuchangamkia fursa za mafunzo kwani baada ya kupata ujuzi utawasaidia kujiajiri wenyewe ama kuajiriwa hali itakayowatoa kwenye utegemezi.

Alifahamisha kuwa wazazi na walezi wana jukumu la kuhakikisha wanawasisitiza na kuwahimiza vijana wao wajiunge na Vyuo vya Amali kwani ujuzi watakaoupata utawanufaisha kimaisha.

Alisema kuwa dira ya maendeleo Zanzibar ya mwaka 2000 hadi 2020 iliweka shabaha ya kuongeza ajira kwenye sekta ya utalii kwa asilimia 50, sekta ya kilimo asilimia 25 na asilimia 30 katika sekta nyengine mchanganyiko.

Balozi Seif alibainisha kwamba shabaha hiyo imekusudia kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira kutoka asilimia 17.1 hadi kufikia asilimia 10 ili pia kuongeza uwezo wa watendakazi kwa nia ya kuchukuwa fursa za ajira pale zinapojitokeza.

Balozi Seif alifahamisha kwamba sera za kitaifa na kisekta zilizopo zinaonyesha jinsi Zanzibar ilivyolichukulia suala la ajira kwa vijana kuwa ni jambo la msingi na muhimu linalohitaji kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa.

Alisema serikali imetekeleza jukumu lake kwa kuwapatia mafunzo vijana hao, kinachofuata hivi sasa kwao ni kuchapa kazi kwa mujibu wa fani walizosomea wakielewa kwamba kazi ni kipimo cha utu mahali popote pale.

Balozi Seif alisema hakuna mtu mwenye jukumu la kubadilisha ustawi wao isipokuwa wao wenyewe kwani maisha mazuri wakati wote yanapatikana kwa kufanya kazi za halali na bidii.

Akizungumzia suala la uchaguzi, aliwapongeza vijana kwa ushiriki wao tulivu katika harakati za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kampeni zinazofikia ukingoni.

Alisema vijana ni sehemu kubwa ya wananchi watakaoshiriki katika kupiga kura kwa kuamini kwamba wote wamejiandikisha na tayari wanavyo vitambulisho vya kupigia kura, hivyo ni vyema wakaitumia haki yao ya kidemokrasia kwenda kuwachaguwa viongozi watakaosimamia maendeleo yao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk. Bakari Ali Silima akitoa taarifa ya mafunzo hayo alisema jumla ya vijana 660 kutoka wilaya 11 za Zanzibar walishiriki mafunzo hayo yaliyolenga kuwapatia ujuzi wa kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.

Alisema   uimarishaji wa mafunzo ya amali chini ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar umejikita katika mfumo wa mabadiliko ya uchumi wa viwanda  kupitia mafunzo ya ufundi wa vifaa vya umeme, ushoni, upambaji na useremala.