ALGIERS,ALGERIA

WANANCHI wa Algeria wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Algiers na maeneo mengine ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wakiadhimisha miaka 32 ya harakati ya kupigania demokrasia nchini humo na kutoa wito wa mabadiliko ya kisiasa.

Maandamano hayo yalifanyika siku mbili tu kabla ya kuanza kampeni ya kura ya maoni ya Novemba Mosi juu ya katiba mpya ambayo Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kwamba itafungua ukurasa mpya kwa nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

Maandamano hayo yaliibuka kwanza katika miji yote ya Algeria mnamo Februari 2019 kupinga mpango wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika wa kugombea muhula wa tano wa urais.

Waalgeria waliendeleza maandamano hayo ya kudai demokrasia na utawala wa kiraia hata baada ya Bouteflika kung’atuka madarakani kwa mashinikizo ya wananchi na wanajeshi wa nchi hiyo.

Mwezi Machi mwaka huu serikali ilipiga marufuku maandamano ya barabarani, ikisema hatua hiyo ilikuwa muhimu kupambana na maambukizi ya janga la corona.

Katika maandamano ya Waalgeria kulisikika nara zinazotaka kujiuzulu serikali ya sasa ya nchi hiyo na kuwepo serikali ya raia.

Waandamanaji hao pia walitaka kuachiliwa huru wanachama wa harakati ya Hirak ya kupigania demokrasia na zaidi ya watu 60, wakiwemo waandishi wa habari, wanaharakati na watendaji wengine wa mashirika ya kiraia wanaoshikiliwa kizuizini kwa vitendo vinavyohusiana na harakati za maandamano.