NA HUSNA MOHAMMED

WADAU mbalimbali wa masuala ya kupambana na udhalilishaji na ukatili wa kijinsia wametakiwa kutokata tamaa dhidi ya mapambano hayo, ili kuifanya jamii kuwa salama.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzani (TAMWA) Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, wakati akifungua mkutano wa udhalilishaji.

Alisema kila mmoja anawajibika katika masuala ya udhalilishaji katika jamii hivyo msaada wa hali ni mali katika kufanikisha nguvu za pamoja bado unahitajika.

“Baada ya kuzungumza sana na mara kwa mara kidogo vyombo vya sheria kidogo tumeona mabadiliko na hiki ndio kinachokihitaji kwa kuwa baadhi ya kesi zimechukua muda mfupi sana naomba mzidishe ari hiyo kwa maslahi yetu na watoto wetu ambao ndio wahanga wakubwa wa matukio hayo”, alisema Dk. Mzuri.

Mapema akiwasilisha mada juu ya udhalilishaji, Asha Aboud, kutoka jumuiya ya Action Aid, alisema matukio ya udhalilishaji yanakumbwa na changamoto nyingi hadi kuwatia hatiani walalamikiwa.

“Jamii kutokuwa tayari kutoa ushahidi, kuchelewa majibu ya vinasaba, keshi kuchukua muda mrefu , muhali, uchelewaji wa ufuatiliaji wa kesi pia ni kizingiti”, alisema Asha Aboud.

Hivyo, alisema kila mmoja ni mas-ula katika kufanikisha hilo kwani bila ya ushiriki wa sehemu moja ni wazi kuwa hakuna litakalofikiwa.

Mapema washiriki wa mkutano huo, walitupia lawama vyombo vya sheria kwa kuchelewesha kesi za udhalilishaji na hivyo jamii kukata tamaa hasa kwa waathirika wa kesi hizo.

Akitoa ushuhuda Asha Omar, ambae mtoto wake wa miaka 13, alibebeshwa ujauzito mwaka 2019 alisema tangu aliporipoti kesi hiyo kumekuwa na ukimya mkubwa kwa vyombo vya sheria kujua hatua iliyofikiwa.

“Tangu mwanangu mjamzito, mpaka sasa ameshajifungua na mtoto ameshachangamka naambiwa subiri, utaitwa, tunafuatilia, nasema kwa uchungu mkubwa kikao hichi leo kitanipa jibu sina Imani na vyombo vya sheria”, alisema huku machozi yakimtoka.