BISHKEK, KYRGYZSTAN

WANANCHI wa Kyrgyzstan wanaopinga matokeo ya uchaguzi wa bunge wamevamia makao makuu ya serikali na majengo ya usalama wa taifa pamoja na bunge mapema jana.

Hayo yaliripotiwa na tovuti za nchi hiyo za Akipress na 24.kg. Baada ya kuyavamia majengo hayo, maelfu ya waandamanaji walimuachia huru rais wa zamani wa Kyrgyzstan, Almazbek Atambayev na maofisa kadhaa wa zamani wa ngazi za juu.

Rais wa Kyrgyzstan, Sooronbai Jeenbekov alisema  atakutana na viongozi wa vyama vyote ambavyo vilishiriki katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita.

Kituo cha Radio Free Europe, kimechapisha picha kwenye ukurasa wake wa Twiiter zikiwaonyesha waandamanaji wakiwa kwenye ofisi ya Jeenbekov, kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bishkek.

Mwaka huu, Atambayev alihukumiwa kifungo cha muda mrefu gerezani, kwa tuhuma za rushwa baada ya kutofautiana na mrithi wake.