NA AMEIR KHALID, DAR ES SALAAM

WAANDISHI wa habari wameshauriwa kujifunza na kujiunga na taaluma ya huduma ya kwanza kwani ina umuhimu mkubwa katika kazi zao.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa chama cha msalaba mwekundu (Red Cross) Tanzania Julius Kejo wakati wa mkutano uliowashirikisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika ofisi za chama hicho, Mikocheni.

Alisema kuna umuhimu kwa waandishi wa habari kusoma taaluma hiyo, ambayo itawasaidia katika kazi zao za kila siku na jamii inayowazunguka.

Alisema waandishi wakiwa na taalamu hiyo itawasaidia kufanya kazi zao kwa umakini na kujikinga na hali mbalimbali za dharura wanapokuwa kazini.

Kejo alisema hivi sasa, Red Cross inakamilisha mpango mkakati wa miaka mitano, utakaofanikisha malengo ya kuhakikisha wanajitegemea badala ya kutegemea wafadhali.

Nao baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo walielezea kufarajika kwao kwa kupata elimu ambayo hapo awali walikuwa hawaifahamu.

Walisema baada ya kupata elimu hiyo, watajitahidi kuandika makala na habari zinazohusu huduma ya kwanza pamoja kwa kuandaa na kutoa vipindi tofauti.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Red Cross, John Busungu alisema mbali na taasisi hiyo kutoa huduma katika majanga mbalimbali, pia inatekeleza miradi ya kusaidia jamii.

Aliitaja baadhi miradi hiyo kuwa ni kuchimba visima katika mikoa mbalimbali, kutoa huduma katika kambi za wakimbizi na kuwaunganisha wanafamilia ambao walipoteana kwa miaka mingi.