NA ABOUD MAHMOUD

WADAU wanaotoa msaada wa kisheria Zanzibar wametakiwa kutoa mashirikiano kwa sekta mbalimbali za kisheria ili kufanikisha upatikanaji wa haki kwa jamii.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara ya Msaada wa Kisheria, Hanifa Ramadhan Said wakati akifungua mkutano wa siku moja wa kukusanya maoni ya kuzipitia rasimu ya ripoti ya mwaka ya msaada wa kisheria katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Mkurugenzi huyo alisema, ushiriki wa wadau hao utasaidia kuondosha matatizo  yanayowakabili wananchi wakiwa ni walengwa muhimu katika kukwamua matatizo yao.

Alisema ni vyema wadau hao wa sheria kuitumia siku hiyo kwa kuingiza na kutoa maoni yao kwa ajili ya kuimarisha rasimu na tathmini ya awali ya hali halisi ya msaada wa kisheria Zanzibar.

“Wito wangu kwenu wadau wa sheria kuitumia siku hii ya leo kutoa maoni yenu ambayo yatasaidia kuhakikisha yale tuliyoyakusudia kwa maslahi ya wananchi yanatimia,” alisema.

Hanifa alisema lengo la kuandaliwa mkutano huo ni kuimarisha rasimu ya tathmini na hali halisi ya msaada wa kisheria kwani wasaidizi hao wana umuhimu katika jamii katika kuleta maendeleo.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema ana imani kubwa na wasaidizi hao wa kisheria kwamba watatoa mawazo yao na yatakwenda kufanyiwa kazi ili baadae aweze kukabidhi nyaraka nzuri kwa wananchi yenye msaada na umuhimu kwa wananchi wa Zanzibar.

Naye Mratibu wa Shirika la mipango ya maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Zanzibar, Salma Ali Hassan alisema kufanyika mkutano huo kwa wadau wa msaada wa kisheria ni jambo muhimu kwani bila kufanya tathmini hakuwezi kupatikana mafanikio.

“Kufanywa mkutano kama huu ni jambo muhimu sana, kwani bila kufanya tathmini hatuwezi kujua wapi tulipotoka na wapi tupo katika kuleta maendeleo yetu wenyewe na kujiondoshea matatizo yanayotukabili,” alifafanua.

Aidha Mratibu huyo alitoa pongezi kwa wadau wa msaada wa kisheria Zanzibar kwani alisema bila ya wao malengo yaliyokusudiwa hayatofikiwa.

Alifahamisha kwamba wadau hao ndio wanaokutana na walengwa na kuwaeleza matatizo yao yanayowakabili na nini wanahitaji ili kutatua na kupatikana wanachokitaka.

Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha wadau wa msaada wa kisheria kutoka katika taasisi mbali mbali zikiwemo za serikali na za binafsi kutoka Unguja na Pemba.