NA ABOUD MAHMOUD

WACHEZAJI wa mchezo wa Kriketi Zanzibar wameiomba serikali kuwaunga mkono ili kurudisha hadhi ya mchezo huo kama ilivyokuwa awali.

Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili katika mazoezi ya mchezo huo katika uwanja wa Mnazi Mmoja, walisema mchezo hivi sasa hadhi ya mchezo huo imeshuka na kudharauliwa na wanamichezo wengi kutoupa nafasi.

Mchezaji Dinesh Kumar, alisema hivi sasa mchezo huo umekuwa hauna wachezaji kutokana na kutoungwa mkono wataasisi mbalimbali zinazohusiana na michezo tofauti na timu za mchezo huo Tanzania Bara.

“Hatuna mashindano, hatuna wachezaji wala hatuungwi mkono na mtu wala Idara yoyote, tunajikusanya sisi wenyewe na kufanya mazoezi kwa sababu huu mchezo tunaupenda,” alisema Dinesh.

Nae Kuldip Meisuria alisema miaka ya nyumba walisikia kuwa mchezo huo visiwani Zanzibar ulikua maarufu na kufanikiwa kushiriki katika mashindano mbalimbali kwa kuchanganyika wachezaji wa makabila tofauti tofauti na sasa hivi.

Alisema ni vyema Serikali kupitia wizara inayohusika na michezo ikaingilia kati na ili mchezo huo urudi katika hadhi yake na kuitangaza nchi kitaifa na kimataif.

 “Tunasikia hadithi kutoka kwa wazazi wetu kwamba kuanzia miaka 1950 mpaka 1970 mchezo huu ulikua na hadhi kubwa sana hapa Unguja, wachezaji wa makabila mbalimbali walicheza na hakukua na ubaguzi na serikali ilishirikiana nao,” alisema.