NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA ya mkoa Vuga chini ya Hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira amewahukumu kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka Saba vijana wawili kwa kosa la kuvunja nyumba usiku.

Vijana hao ni Ahmed Khatib Ali (22) mkaazi wa Sogea na Rashid Ali Juma (21) mkaazi wa Sebleni, wote kwa pamoja walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja nyumba na kufanya wizi ndani ya nyumba Rehema Juma Othman.

Adhabu kwa washitakiwa hao imetolewa kufuatia mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Hakimu Hamisuu, alisema kosa la kuvunja watumikie Chuo Cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitatu huku kwa kosa la wizi watumikie miaka minne na  aliamuru adhabu kwa washitakiwa hao ziende sambamba.

Upande wa Mashitaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Mohammed Abdalla, uliwasilisha mashahidi sita akiwemo mama aliyefanyiwa tukio hilo.

Kabla ya adhabu aliiomba Mahakama kutoa adhabu Kali kwa mujibu wa Sheria, ili vitendo vya wizi vipungue.