NA HUSNA SHEHA

MAHAKAMA ya Mkoa Mahonda chini ya Hakimu Faraji Shomari Juma, amewahukumu kutumikia Chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka kumi vijana wawili kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya zenye uzito wa 987.719g.

Vijana hao ni Mabula Mohammed Mbako (45) mkaazi wa Mangapwani na Dadi Mussa Rehani (24) mkaazi wa Bumbwini Wilaya ya Kaskazini ‘B’Unguja, wote hao walifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kupatikana na dawa wa kulevya.

 Adhabu hiyo imetolewa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na mahakamani hapo.

Upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Ali Juma, iliwasilisha mashahidi wanane akiwemo mkemia wa serikali.

Hata hivyo, upande wa mashitaka umedai kuwa hakuna kumbu kumbu za makosa ya zamani  na kuiomba mahakama itowe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ya kosa linalo wakabili.

Kabla ya kutolewa adhabu, Mahakama iliwapa nafasi ya kujitetea ambapo Mabula aliiomba Mahakama impe kifungo cha nje, kwa vile yeye ana familia inamtizama ya mke na watoto, huku mshitakiwa Dadi aliiomba mahakama impunguzie adhabu atakayopewa kwa vile hali yake ni mgonjwa na hairuhusu hilaki za gerezani.