MCHAKATO wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, utahitimika kwa Tume zetu za Uchaguzi Tanzania, ikiwemo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), kutangaza washindi kwenye nafasi mbalimbali zilizowaniwa.

Tume hizo zitatangaza matokeo ya walishinda kwa nafasi ya udiwani, ubunge, uwakilishi na waliomba nafasi kubwa za kiutendaji za urais wa Zanzibar na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua ya kutolewa matokeo ya uchaguzi kwa wagombea maana yake ni kumalizika kwa zoezi zima la uchaguzi na kinachofuata ni nafasi ya waliochaguliwa kulishwa viapo na kwenda kuwatumikia wananchi kwenye nafasi zao.

Kwa wakati huu tukiwa na shauku baada ya kupiga kura  ni vizuri pia tukajiandaa kisaikolojia kuyapokea matokeo.

Zoezi la uchaguzi lazima litoe mshindi mmoja hata kama nafasi iliyokuwa ikiwaniwa ilikuwa na washindani 20, suala ambalo kwa uzoefu wetu wakati mwengine linaleta ukakasi kwa baadhi ya watu kukubaliana na matokeo.

Wapo wagombea watakao susia matokeo, wapo watakao dai kutoyatambua matokeo, wapo watakao utia doa uchaguzi mzima kwa sababu tu hawakushinda wao.

Wagombea wa namna hii watajenga hoja dhaifu zinazolenga kutuaminisha kuwa uchaguzi ulikuwa mbaya na wenye kasoro nyingi kwa sababu kura hazikutosha kwa upande wao.

Wanasahau kuwa waliofanya uamuzi wa zoezi la kura ni wananchi ambao kwa upeo wao wamewapima wagombea wote baada ya kusikiliza sera na hatimaye kwa kauli moja kuchagua mgombea mmoja kwa kumpa kura nyingi.

Tunaelewa kushindwa kunasababisha hasira, ghadhabu na hamaki, lakini kama uliingia kwenye mchezo wa uchaguzi, lazima ukubaliane na kanuni za uchaguzi kwa maana kwamba kama hukuchaguliwa bahati haikuwa kwako.

Pia tunapaswa kukumbuka kuwa cheo ama dhamana yoyote msingi wa kuipata kwake hakutokani na kuigombea ama kuiwania, bali nafasi hiyo na nyengine mgawaji wake ni Mwenyezi Mungu. 

Kwa upande wengine watakuwepo mashabiki na wapambe wa wagombea na vyama nao watazusha yao, watasambaza mikakati potofu katika jamii aliyeshinda kafanya hivi ama kafanya vile.

Matokeo yake ni kushuhudiwa wafuasi wa walioshinda kususiwa kwa kutoshirikishwa kwenye mambo ya kijamii, ikiwemo hata pengine wasipakiwe kwenye gari za abiria kwa sababu ni wafuasi wa mtu aliyeshinda.

Kwa hakika haya sio mambo mazuri na tusingependa kuyaona yanatokea na badala yake zoezi la mchezo wa uchaguzi linapokwisha tuunde timu moja ambayo tuipe jina la uzanzibari itakayotusaidia kuvijenga visiwa vyetu kwa nguvu zetu wenyewe.

Haipendezi kabisa kwa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao wanaabudia dini moja, kitabu chao kimoja, mtume wao mmoja, na hata kibla chao kimoja wanasusiana na kuhasimiana kwa sababu ya uchaguzi.

Tuuchukulie uchaguzi ni zoezi la kubadilisha uongozi wa juu katika nchi yetu, lakini jambo zuri zaidi ni kwamba aliyeshinda si mtu wa wafusi wake tu, bali anakuwa kiongozi wetu sote wananchi za Zanzibar.

Kama aliyeshinda ni kiongozi wetu sote kwanini tuhasimiane, kwanini tusiombane chumvi, kwanini tusishirikiane kwenye misiba na harusi? Tusiendekeze vitendo vya kishetani ambaye kila tunapofanya maovu ndiyo furaha kwake.

Tuishie kusema tujiandae kisaikolojia kupokea matokeo, kujiandaa kwetu huko tufikirie tunu ya amani iliyojaaliwa nchi yetu, ambapo kama itatutoka kutakuwa na gharama kubwa za kuirejesha.