NAIROBI,KENYA

MIUNGANO mbalimbali ya wahudumu wa afya jijini Nairobi imeomba   hadi Octoba 29 kwa Wizara ya Afya na Tume ya Huduma za umma, kushughulikia matakwa yao la sivyo watasitisha huduma kwenye hospitali zote za umma.

Miungano hiyo ililalamikia kupuuzwa kwa mikataba ya makubaliano baina yao na serikali ya kaunti huku wanachama wakiendelea kutaabika hasa wakati huu wa janga la corona.

Miongoni mwa matakwa wanayoshinikiza yatekelezwe ni pamoja na kupandishwa vyeo, kuongezewa mishahara na marupurupu na kupewa mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Viongozi wa miungoni hiyo zikiwamo KPMDU za madakatari, wauguzi KUNU, na CUCO ya maofisa wa kliniki walitaka Wakenya kutotafuta huduma za matibabu katika Hospitali za umma ifikapo Octoba 29.

Haya yanajiri huku Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nakuru walilalamikia mazingira duni ya kufanyia kazi huku wakitishia kusitisha huduma iwapo matakwa yao hayatoshughulikiwa kwa haraka.

Wauguzi hao walisema kwamba Serikali ya Kaunti ya Nakuru iliwatelekeza huku wenzao ishirini na wawili wakiambukizwa virusi vya corona kutokana na ukosefu wa vifaa vya kujikinga wanawapowahudumia waathiriwa wa corona.

Wakizungumza wahudumu hao walisema kuwa kaunti ilikataa kuwapa mafunzo ya kukabili maambukizi ya corona hali inayowaweka katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa.

Aidha wanashinikiza shughuli ya kuwafuatilia waliotangamana na waathiriwa kufuatiliwa na kuwekwa karantini.

Vilevile, waliuomba usimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Nakuru kuhakikisha kuwa wagonjwa wanoingia hospitalini humo kutibiwa wanapimwa kubaini iwapo wanavirusi vya corona au la.