NA HAFSA GOLO
WANAFUNZI wamesifu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya awamu ya saba katika suala zima la kuimarisha michezo maskulini sambamba na kuienzi siku ya elimu bila malipo.
Walisema kitendo cha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kutilia mkazo suala la michezo maskulini kimeongeza mwamko na hamasa za wanafunzi kutambua historia, mila na silka zao katika maswala ya tamaduni na michenzo.
Akizungumzia hatua hiyo, mwanafunzi Khamis Juma aliishauri serikali ya awamu ya nane kundeleza azma ya mapinduzi ya kuwapatia vifaa na walimu wenye taaluma ya michezo.
“Hivi sasa hamasa na ushindani baina ya skuli na skuli katika sekta ya michezo imerudi kama ilivyokuwa zamani jambo ambalo limesaidia wanafunzi wengi kushiriki katika michenzo,” alisema Juma.
Alisema hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa wachezaji wazuri ambao wataitangaza Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Nae Habiba Juma alisema, kitendo cha serikali kuhamasisha michenzo skulini kimesaidia kujenga afya za wanafunzi na kushiriki vyema masomo yao.
“Mazoezi ni tiba bora kwa binaadamu, unaposoma unatakiwa uwe na muda wa kupumzisha akili hivyo michezo itatusaidia sana wanafunzi,” alisema.
Juma Daudi alisema, Dk. Shein ameona umuhimu wa wanafunzi kushiriki katika sekta ya michezo kwani ndio moja ya msingi mzuri wa kuwajengea uwezo na kutimiza malengo waliojiwekea.
“Tunasikia kwamba wapo baadhi ya viongozi wakubwa nchini walikuwa wanamichezo wa zuri akiwemo Rais wetu wa awamu ya saba hivyo suala la michezo ni muhimu hakukosea kulihimiza,” alisema.
Siku ya elimu bila ya malipo huadhimishwa kila ifikapo Septemba 23 kwa tamasha maalum la michezo, utamaduni na shughuli za kitaaluma ambapo kwa mwaka huu Zanzibar iliadhimisha miaka 56.