YERUSALEMU, ISRAEL

MAELFU ya Waisrael wameandamana usiku kote Israeli dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, wakiendelea na kampeni yao dhidi ya kiongozi huyo licha ya Serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya watu katika juhudi mpya za kuzuia kuenea maambukizi ya virusi vya corona.

Netanyahu alisema marufuku hiyo ni kwa lengo la kulinda usalama wa raia, waandamanaji wanamshutumu kwa kutaka kukomesha harakati zao.

Waandamanaji hao walikuwa wakikusanyika nje ya nyumba ya Netanyahu mjini Jerusalem kila wiki kwa zaidi ya miezi mitatu, wakimtaka ajiuzulu.

Waandamanaji wanasema Netanyahu hapaswi kuwa waziri mkuu wakati anashitakiwa kwa madai ya ufisadi.

Aidha wanamlaumu pia kwa kushindwa kuushughulikia ipasavyo mgogoro wa virusi vya corona, ambao uliharibu uchumi wa nchi hiyo.

Wengi wa waandamanaji ni Waisrael vijana ambao walipoteza kazi kutokana na janga hilo.