NA  AZIZI SIMAI, PEMBA

NAIBU Waziri wa Kazi , Uwezeshaji, Wazee , Wananawake na Watoto Zanzibar, Shadia  Moh’d Suleiman, amewataka, wajasiriamali wanaopewa mikopo kupitia Wizara hiyo, kurejesha mikopo wanayopatiwa kutokana na masharti waliyopewa wakati walipokuwa wakikabidhiwa mikopo hiyo.

Shadia alisema, lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo kwa wajasiriamali

na wafanya biashara wadogo wadogo ni kuwapa msukumo wa kuendelesha shughuli zao bila ya pingamizi zozote ili feha hizo ziweze kurejeshwa kwa wakati na kusaidia wengine. Naibu Waziri huyo alieleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na wajasiriamali wa  kilimo cha mboga mboga na wafanyabiashara ambao wamebahatika kupata mikopo ya fedha kwa kipindi hichi huko katika ukumbi wa Ofisi ya Wizara Kazi,uwezeshaji, wanawake na watoto Pemba.

“ Fedha munazopatiwa ni kwa ajili ya kuendeleza biashara zenu ndogo ndogo , ili ziweze kuwakombowa kiuchumi na sio sadaka munatakiwa muzitumie na murejeshe na wengine wafaidike,” alieleza. Alifahamisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja (1bilion) zimekopeshwa wajasriamali kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo cha mboga mboga na biashara ikiwa ni juhudi za Serikali kwa ajili ya kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha ili waweze kujiajiri.

Shadia alieleza,  lengo la wizara hiyo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi ili waweze kujitegemea ambapo jumla ya wajasriamali 644,walishafaidika na mikopo hiyo ikiwemo mboga mboga na biashara ndogondogo.

Naye Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Suleiman Said  Moh’d aliwataka wakulima hao kuwatumia wataalamu wa kilimo wakati wa kulima na kupanda ili waweze kupata mavuno mazuri na kujitahidi kutumia dawa na mbolea baada ya kupata maelekezo ya kitaaluma.