NA KHADIJA KHAMIS, MAELEZO

MKUU wa Operesheni na Haki za Binaadam kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Haji Faki Hamduni, amesema mashirikiano ya pamoja yanahitajika kati ya Wakuu wa Madiko, Halmashauri za Wilaya na Kamisheni katika kupokea taarifa za haraka inapotokea tatizo .

Akizungumza na Wakuu wa Madiko wa Wilaya ya Kusini Unguja katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini, Kitogani, baada ya kupokea changamoto za wavuvi na wakulima wa mwani  zinazowakabili katika ufanyaji wa kazi zao.

Amewashauri wavuvi kuzingatia taarifa za Mamlaka ya hali ya hewa kabla ya kwenda baharini na kujenga mtandao wa mawasiliano wa pamoja wakiwa baharini, ili kuweza kusaidiana panapotokezea matatizo ya ghafla.

Alifahamisha kuwa taarifa za Mamlaka ya hali ya hewa zimeeleza kuwa mvua za vuli zinategemewa kuwa za wastani, lakini mabadiliko yeyote yanaweza kutokea hivyo Wavuvi na wakulima wa mwani pamoja na kamati zao kuwa na tahadhari zaidi, ili kujiweka tayari na athari za maafa zinazoweza kujitokeza .

Nae Afisa Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Kusini, Haji Mtego Hassan, ameeleza kuwa eneo kubwa la bahari ya Wilaya ya kusini ikiwemo Michamvi, Bwejuu, Paje na Makunduchi hakuna Kituo cha Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo jambo ambalo linachangia  kukosa msaada wa haraka wa uwokozi wakati wa ajali ya bahari inapotokea .

Aidha, alifahamisha kuwa elimu ya athari za bandari bubu zinaendelea kutolewa kwa wahusika na  inasaidia kuthibiti uingiaji wa wageni kiholela kupitia njia hizo.

Mkuu wa Diko la Jambiani Kibigija, Omar Mpango Simai, amesema kuna umuhimu wa kutoa taarifa za hali ya hewa mara kwa mara, ili kujuwa mabadiliko yanapotokea .