NA TATU MAKAME

WAFANYABIASHARA wa dagaa katika eneo la Mangapwani, mkoa wa Kaskazini Unguja, wamelalamikia fedha wanazotozwa na wamiliki wa mashamba wanayotumia kuanikia dagaa kwani unapunguza mapato na kuwaondolea utulivu wa kibiashara.

Wafanyabiashara hao walisema hayo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika eneo la biashara hiyo hivi karibuni.

Walisema wamiliki wa mashamba wamekuwa wakiwalipisha kodi kila mwaka hali inayopelekea kushindwa kukidhi mahitaji yao lakini pia kumudu gharama za biashara hiyo.

Walisema mbali na kodi ya mashamba, pia wanalipia tozo mbali mbali ikiwemo kulipia ving’amuzi vya kuchemshia dagaa hali inayopelekea usumbufu na kuwaongezea mzigo.

Mmoja ya wafanyabiashara hao, Mwajuma Simai Haji, wa Kijiji cha Fujoni, wilaya ya Kaskazini ‘B’ na Tatu Ali Haji wa Kiembesamaki, wilaya ya Magharibi ‘B’ walisema kodi zisizo rasmi zimekuwa zikiwakosesha mapato yenye faida kutokana na biashara kiasi cha kupelekea kushindwa kuendelea na kazi hiyo kwa misimu mengine.

“Ingawa tunaendelea na hii kazi, lakini kodi imekuwa kikwazo kikubwa na kupelekea usumbufu unaotutia umaskini badala ya kujikwamua nao,” alieleza Mwajuma Simai Haji.

Wakizungumzia malalamiko ya wafanyabiashara hao, wamiliki wa mashamba hayo walisema wanalazimika kutoza fedha hizo kutokana na kubadilisha matumizi ya maeneo hayo ambayo awali waliyatumia kwa kilimo.

Walisema kutokana na hali hiyo hawawezi kuwaachia waanika madagaa bila kuwatoza kodi, kwani wanayategemea maeneo hayo kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.

“Tumebadilisha matumizi, tulikuwa tunalima na tumeona wakati wafanyabiashara wa dagaa wanayahitaji maeneo haya bora tuwakodishe,” alisema.

Akizungumza na wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wadogo wa eneo hilo hivi karibuni, mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema endapo atachaguliwa, atahakikisha anaweka mfumo mzuri wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara ili kuwaondolea usumbufu katika shughuli zao.