NA ASIA MWALIM

JAMII imeshauriwa kutoa elimu ya kupinga vitendo vya udhalishaji wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo kwa vizazi vya sasa na baadae.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Madrasa wanaopinga vitendo vya udhalishaji Zanzibar, Omar Said Rajab alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Mfenesini, wilaya ya Magharibi ‘A’, Zanzibar.

Alisema vitendo vya udhalishaji nchini vimekua changamoto inayowakabili watoto na taifa kwa ujumla, hivyo ipo haja ya kuendelea kupingwa kwa kila mmoja kwa vitendo.

Alieleza kuwa licha ya jitihada za serekali kukabiliana na vitendo hivyo, baadhi ya taasisi kuendelea kutoa elimu ya udhalilishaji mijini na vijijini, bado kuna watu katika jamii wapo nyuma kuibua vitendo hivyo.

“Hivi karibuni tumeshudia mama alieficha uhalifu aliofanyiwa mtoto wake na baba mzazi wa mtoto huyo kutokana na watoto wanahofia kutoa taarifa baada ya kutishwa hivyo hushindwa kusema chochote,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema Jumuiya hiyo imejipanga kutoa elimu hiyo hasa kwa wanafunzi kwani ndio wanakutwa na kadhia hizo mara kwa mara pindi wanapokua katika harakati zao za masomo.

Alifahamisha kuwa hali ya vitendo vya udhalishaji imekithiri kwenye maeneo rafiki ya wanafunzi ikiwemo skuli, madrasa, ambapo ni sehemu inayotakiwa kupata elimu wakiwa na amani.

“Tutatoa taaluma kupita kwenye skuli na madrasa za kurani ili wanafunzi wasisite kusema pale watakapo kumbwa na kadhia hiyo,” alisema.

Nae Katibu wa jumuiya hiyo, Nyanzige Saidi Yatabu, alisema mara nyingi mafunzo yanayotolewa hayawafikii walengwa, hivyo ni vyema kuwepo utaratibu maalumu wa kufikisha ujumbe ili kuondokana na ongezeko la vitendo hivyo.

“Ili tupate viongozi bora wa badae inatupasa kuwalea, kuwatunza, pia kuwajenga wawe na hofu ya Mwenyezi Mungu kwani watoto ndio taifa la kesho,” alisema.