NA LAILA KEIS

IMEELEZWA kuwa serikali ya awamu ya saba imepiga hatua kubwa kuimarisha sekta ya elimu, ikiwa ni utekelezaji wa dhana ya elimu bora nchini.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Khalid Abdalla Omar, aliyasema hayo katika kongamano la kuadhimisha siku ya walimu duniani, lililofanyika katika ukumbi wa kitengo cha uzazi salama, Kidongo Chekundu mjini Zanzibar.

Alisema, serikali kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020, dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 na mkakati wa kukuza uchumi imefanya mambo mengi ambayo yana lengo la kukuza sekta ya elimu.

Aliyataja miongoni mwa mambo hayo kuwa ni kuondolewa kwa michango ya wazazi katika elimu ya msingi kwa mwaka 2015/2016 na kuondoa gharama za mitihani ya sekondari mwaka 2016/2017 jambo ambalo limeshajihisha wazazi kuwapeleka watoto wao skuli.

Awali akimkaribisha mgeni huyo, Rais wa chama hicho Mwalimu, Seif Mohammed Seif, aliishukuru serikali kwa kulisimamia suala la mripuko wa janga la corona, kwani lilisitisha shughuli za elimu kwa muda wa miezi mitatu.

Hivyo aliiomba serikali kurudisha mfumo wa ufundishaji kwani ilivyopangwa baada ya kurudi maskulini kutokana na janga la corona, kunampa wakati mgumu mwalimu katika kumaliza mtaala wake, ambapo mada moja hufundisha zaidi ya mara 3 kwa wanafunzi wa darasa moja.

Pia kupitia kongamano hilo, aliiomba wizara kumkamilishia mwalimu asilimia 25 ya posho ambayo anatakiwa kulipwa, ambayo kwa sasa hawaipati.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika wilaya ya mjini, Mkurugenzi Msaidizi Baraza la Manispaa Mjini, Kibibi Mohammed Mbarouk alisema, wanaishukuru serikali kwa kuongeza ajira kwa walimu, jambo ambalo limeongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Naye Msaidizi Mkurugenzi Elimu Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’, Hassan Abass Hassan, alisema katika kipindi cha miaka 10 ya Dk. Shein, sekta ya elimu imefanikiwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya madarasa na upatikanaji wa vikalio.