NA LAILA KEIS
IMEELEZWA kuwa serikali ya awamu ya saba imepiga hatua kubwa kuimarisha sekta ya elimu, ikiwa ni utekelezaji wa dhana ya elimu bora nchini.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Khalid Abdalla Omar, aliyasema hayo katika kongamano la kuadhimisha siku ya walimu duniani, lililofanyika katika ukumbi wa kitengo cha uzazi salama, Kidongo Chekundu, Zanzibar.
Alisema, serikali kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020, dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 na mkakati wa kukuza uchumi imefanya mambo mengi ambayo yana lengo la kukuza sekta ya elimu.
Aliyataja miongoni mwa mambo hayo kuwa ni kuondolewa kwa michango ya wazazi katika elimu ya msingi kwa mwaka 2015/2016 na kuondoa gharama za mitihani ya sekondari mwaka 2016/2017 jambo ambalo limeshajihisha wazazi kuwapeleka watoto wao skuli.
“Serikali imeongeza uandikishaji wa watoto katika ngazi ya elimu ya lazima, ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari kutoka wanafunzi 31,7278 kwa mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 52,9688 kwa mwaka 2020,” alisema.
Awali akimkaribisha mgeni huyo, Rais wa chama hicho Mwalimu Seif Mohammed Seif, aliishukuru serikali kwa kulisimamia suala la mripuko wa janga la korona, kwani lilisitisha shuguli za elimu kwa muda wa miezi mitatu, kipindi ambacho kiliathiri sekta hiyo, ambapo kwa sasa Shuhuli za elimu zinaendea kama kawaida.
“Tangu kufunguliwa kwa skuli tarehe 29 june, mpaka leo tarehe 5 Oktoba, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake hakujaripotiwa tukio lolote la korona,” alisema.
Hivyo aliiomba serikali kurudisha mfumo wa ufundishaji kwani ilivyopangwa baada ya kurudi maskulini kutokana na janga la korona, kunampa wakati mgumu mwalimu katika kumaliza mtaala wake, ambapo mada moja hufundisha zaidi ya mora 3 kwa wanafunzi wa darasa moja.