NA LAILA KEIS

WAKUFUNZI wa elimu wametakiwa kuhakikisha walimu wanapata fursa ya kujiendeleza kielimu, ili kuleta maendeleo katika sekta hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdalla Mzee, aliyasema hayo wakati wa sherehe ya mahafali ya tano ya elimu masafa, kwa walimu waliohitimu ngazi ya cheti daraja la 3 ‘A’, yaliofanyika katika ukumbi wa skuli ya Ali Hassan Mwinyi, huko Bububu Wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja.

Aidha, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazidi kuboresha sekta hiyo kwa kutoa mazingira mazuri kwa walimu, ili wanafunzi wapate elimu iliyobora zaidi.

“Ndani ya mwaka huu serikali imeajiri walimu 1,500, tumejenga skuli za kisasa 24 ndani ya miaka mitano, pia imefuta michango ya wanafunzi” alisema Naibu huyo.

Sambamba na hilo aliwataka wahitimu hao ambao wametokea kituo cha Kitogani, Mkwajuni, Dunga, Kiembe Samaki na Bububu, kuhakikisha wanamaliza malipo ili waweze kupata vyeti vyao ambavyo vitawawezesha kupata ajira pia kujiendeleza na taaluma hiyo kwa ngazi ya diploma.

Nae Mkurugenzi Idara ya Mafunzo ya Ualimu, Maimuna Fadhil Abas, aliwataka wahitimu hao kufanya kazi kwa bidii, na kuitumia elimu waliyoipata katika kuleta mabadiliko ya usomeshaji, ili kuiweka sekta ya elimu mahala inapotakiwa.

Mmoja ya wahitimu hao kutoka kituo cha TC Dunga, Maryam Abdallah, aliishukuru serikali kwa kuwawekea elimu masafa ambayo inawapatia taaluma zaidi ya usomeshaji, na aliiomba serikali kuwapatia ajira walimu wanaojitolea kwa muda mrefu.

Hayo yalikuwa ni mahafali ya tano ya elimu masafa, ambayo yalikuwa na wahitimu wanawake 501 na wanaume 28 kwa Unguja na Pemba.