NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya Wilaya Mwanakwerekwe, imeiahirisha kesi inayowakabili watu wawili waliodaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udangayifu hadi Novemba 23, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Asya Abdalla Ali, alifikia hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Nyasi Kombo, kuiomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo.

Washitakiwa hao ni Iddi Mkubwa Nassor (47) mkaazi wa Bububu na Ali Mmanga Omar (32) mkaazi wa Tomondo wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja walipatikana na kosa la kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu cha 301 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Walidaiwa kuwa Aprili 10, mwaka jana majira ya saa 11:30 jioni huko Tomondo, wote kwa pamoja walijipatia shilingi 9,000,000 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Said Abdallah Said kwa kumuuzia banda ambalo hawalimiliki kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Washitakiwa hao wapo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kujidhamini wenyewe kwa shilingi 1,000,000 kila mmoja na kila mshitakiwa aliwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja alidhaminiwa kwa shilingi 500,000 za maandishi.