NA TATU MAKAME

WATU watatu wanaendelea na matibabu katika Hospitali kuu ya Rufaa ya Mnazi mmoja baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari huko Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Abdalla Haji alithibitisha tukio hilo na kusema ajali hiyo ilitokea Oktoba 13 mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku.

Alisema ajali hiyo ilihusishwa na gari yenye namba za usajili Z.425 Town ace Private iliyokuwa ikiendeshwa na Abdul-hamid Haji Mohamed (18) mkaazi wa Kombeni Wilaya ya Magharibi ‘B’ ambae ni dereva.

Alisema siku hiyo dereva huyo alikuwa akitokea upande wa Mahonda kuelekea Kitope na kufika hapo gari ilimshinda na kupinduka kisha kuingia kwenye mtaro na kuwagonga watu watatu waliokuwa pembezoni mwa barabara.

Aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Abdul-hamid Haji na Mohamed Ame, wote wakaazi wa Kazole ambao waliumia sehemu mbalimbali za miili yao.

Hata hivyo, alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na wanaendelea na matibabu.

Kuhusiana na tukio hilo, Kamanda Haji, aliwataka madereva kuwa makini wakati wanapoendesha vyombo vya moto, ili kuepusha ajali na wananchi kuwa makini wakati wanapokuwa barabarani.

Nao mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Haji Omar Hijja na Ali Shauri Mustafa, wakaazi wa Kazole, walilitaka jeshi la Polisi kuendelea na utaratibu wa kutumia chombo cha kuangalia mwendo, kwani madereva wamekuwa wakiendesha vyombo vya moto kwa mwendo mkubwa  hasa tangu kujengwa kwa barabara hiyo.