NA SAIDA ISSA, DODOMA

OFISA Masoko wa jiji la Dodoma, James Yuna, amewataka wafanyabishara ndogo ndogo maarufu (Wamachinga) wanaofanya biashara  kwenye maeneo mbalimbali ya jiji kuhakikisha yanakuwa katika mazingira safi badala ya kusubiri kufanyiwa.

Yuna alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabishara hao wakati akikagua maeneo wanayofanyia biashara yaliyopo ndani ya jiji la Dodoma, ambao aliwataka kuhakikisha yanakuwa safi badala ya kungoja kufanyiwa na watu wengine.

Alisema baadhi ya wamachinga wana changamoto ya kutofanya usafi kwenye maeneo yao hata kama kuna faida ambayo wanayoipata ya kujipatia kipato kutokana na biashara zinazofanywa.

“Nimejionea mwenyewe baadhi ya maeneo ambayo wamachinga wamekuwa wakifanya biashara zao, siyo rafiki kwa kufanya shughuli zao, kutokana na hali ya mazingira kuwa ni hayaridhishi kwa kufanya biashara”alisema Yuna.

Katika hatua nyingine akizungumza na wamachinga hao pia amewataka kutoa ushirikiano na taasisi na watu binafsi wanaojishughulisha na suala zima la kuliweka jiji katika hali ya usafi.