NA LAILA KEIS
WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi, wamesema wameridhishwa na kampeni za mgombea urais kupitia chama hicho, Dk. Hussein Mwinyi, kutokana na ahadi zake za kuleta kasi ya maendeleo nchini.
Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti walipokua wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kufuatia kuelekea siku ya kupiga kura.
Walisema wana imani kubwa na Dk. Mwinyi, kuwa mara baada ya wananchi kumchagua na kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, ataitumikia nafasi hiyo kwa kutekeleza vyema ilani ya chama hicho sambamba na kutimiza ahadi alizoweka kwa wananchi wake.
Katibu wa CCM wilaya ya Amani, Ali Salim Suleiman, alisema Dk. Mwinyi amelelewa vizuri katika chama hicho, pia ameonesha uadilifu wa kazi zake katika kuitumikia serikali.
“Mbali ya kuitangaza ilani ya chama ya mwaka 2020/2025 lakini pia nina imani ya asilimia 100 atatimiza ahadi zote alizoziahidi katika kampeni zake” alisema.
Naye Katibu Mwenezi wa Wadi ya Kilimahewa, Fatma Bakar Mohammed alisema kampeni zake za kutembelea makundi mbali mbali katika jamii, zimewapa matumaini wanawake, kuwa wamepata mtetezi atakaetetea haki zao ipasaavyo, kwani dhamira yake ni kuwasikiliza na kuwatumikia.
Mwenyekiti wa wazazi CCM wilaya ya Amani, Seif Amir Seif, aliishukuru serikali kwa kusimamia suala zima la amani na kuhakikisha usalama wa viongozi na wananchi wake ili kuhakikisha kampeni zimemaliza kwa salama.
Naye mkaazi wa Chumbuni, Haji Khamis Haji alisema, kutokana na kuvutiwa na sera za Dk. Mwinyi, yeye pamoja na vijana wenziwe walipita nyumba kwa nyumba kushajihisha vijana wenzao kutopoteza haki yao ya msingi na kujitokeza kwa wingi kumpigia kura kiongozi huyo.
Kwa upande wake Sultan Kiherehere mkaazi wa Amani alisema, sera za Dk. Mwinyi zimefunua masikio ya wanachama na wasiokuwa wanachama wa Chama hicho, kwani ni kiongozi msikivu na mpenda watu.
“Kampeni zake za kistaarabu zimewafanya wengi kumkubali, kutokana na ahadi zake ambazo zimewapa matumaini ya kuleta maendeleo ya haraka katika nchi yetu” alisema Kiherehere.