CAIRO,MISRI

MAHAKAMA nchini Misri imewahukumu kifo wanachama sita wa Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya maofisa wa polisi.

Mtandao wa habari wa al Khaleej al Jadid uliripoti habari hiyo na kuongeza kuwa,Jaji wa Mahakama ya Kesi za Jinai ya Zagazig mjini Cairo, Misri alitoa hukumu ya kifo kwa wanachama sita wa Ikhwanul Muslimin na kuwafunga miaka kumi wanachama wengine sita wa kundi hilo.

Mahakama hiyo ilidai kuwa watu hao ni wanachama wa kundi lililopiga marufuku,kuwashambulia maofisa wa polisi,kufanya njama dhidi ya Serikali,kuwafyatulia risasi polisi na kushiriki katika mauaji ya maofisa wawili wa polisi pamoja na kuiba silaha za moto.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa,hukumu hiyo bado si ya mwisho na inasubiri kuidhinishwa na Mahakama Kuu ya Misri.

Kwa miaka kadhaa sasa mahakama za Misri zimekuwa zikitoa hukumu nyingi za vifo hasa dhidi ya wanachama wa Ikhwanul Muslimin.

Taasisi za kisheria zinasema kuwa,sehemu kubwa ya hukumu zinazotolewa dhidi ya wapinzani wa Serikali ya Rais Abdel Fattah el Sisi hazitegemei ushahidi wa kweli,bali zinatolewa kwa malengo ya kisiasa.

Mwaka 2013 viongozi wa Misri waliliingiza kundi la Ikhwanul Muslimin katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.

Ukandamizaji mkubwa wanaofanyiwa viongozi na wanachama wa Ikhwanul Muslimin huko Misri umeongezeka baada ya jeshi kumpindua Mohammad Morsi,rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi huko Misri.