NA ABDI SULEIMAN

OFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, amesema kushirikishwa kwa wanafunzi katika kongamano la Siku ya Maafa duniani, litakuwa ni mwarubaini wa majanga mengine kutokea katika jamii.

Akizungumzia umuhimu wa Makongamano hilo kwa wanafunzi, alisema litaweza kuwasaidia uwezo wao wa kufikiri, namna ya kujenga hoja, pamoja na kuwasaidia katika kujibu mitihani yao ya sayansi jamii.

Aliwataka vijana kutumia nafasi hiyo kwa kuhakikisha jamii inapata elimu ya kukabiliana na maafa, kwani ndiko kwenye majanga mbali mbali, huku serikali ikihitaji wananchi wake kuishi salama.

Aidha, aliwataka wanafunzi kutambua kuwa kazi yao ni kusoma wanapokuwa skuli, kwani serikali imekuwa ikiwapatia huduma mbali mbali, sambamba na kuacha kujiingiza katika vishawishi vya siasa, ikizingatiwa kuwa wakati wao bado haujafika.

Mkuu wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Pemba, Khamis Arazak Khamis, alisema Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, imekuwa ikitoa elimu kwa makundi mbali mbali, ili kujikinga na maafa pamoja na kujuwa athari zake, kwani bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakipuuza taarifa mbali mbali zinazotolewa katika kukabiliana na maafa.

Nao wanafunzi hao waliiyomba Kamisheni hiyo, kuendelea kuwalimisha wananchi kwa kuhakikisha wanafika vijijini katika kutoa elimu hiyo ya kukabiliana na maafa na kuna baadhi ya wananchi vijijini hawajuwi hasa nini maana ya maafa, hivyo ili kupunguza au kutokomeza kabisa yasitokee ni vizuri kufika huko na kuelimisha wananchi.