NA ABOUD MAHMOUD

WASANII NA WANAMICHEZO visiwani Zanzibar wamesema wamepokea kwa furaha ushindi wa Rais Mteule wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi na kujenga matumaini kwa kuwaletea maendeleo katika fani zao hizo.

Wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti wasanii na wanamichezo hao walisema imani yao kubwa kwa kiongozi huyo kubadilisha mfumo wa fani zao hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa kundi la Zanzibar One Modern Taarab, Abdullah Ali Abdullah (Duu), alisema ameupokea kwa furaha na kujenga matumaini ushindi wa rais huyo mteule kutokana na ahadi alizokua akiziahidi wakati wa kampeni.

“Nampongeza sana kwa ushindi wa kishindo alioupata, imani yangu kuwa atatuletea maendeleo ambayo yatasaidia kuwainua wasanii na kuona umuhimu wa kazi zao,” alisema.

Aidha ‘Duu’ aliwashauri wasanii wenzake kumuunga mkono kiongozi huo na kumpa mashirikiano kwa kuhamasisha jamii katika kutenda mambo yatakayosaidia kuinua maendeleo ya nchi na sekta ya Sanaa.

“Tukifanya hivyo tutamsaidia kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi lkaini pia kuongeza umaarufu wan chi yetu duniani kote,” alisema msanii huyo.

Nae Rais wa chama cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambae pia ni Diwani mteule wa wadi ya Kwahani, Mohammed Abdullah Makame ‘Laki’, alisema amepokea kwa furaha ushindi wa Dk. Mwinyi na kumpongeza kwa kupata ushindi huo.

“Namuamini ni kiongozi imara ambae atasimamia wasaniii kuhakikisha wanafikia malengo waliyoyakusudia, nawasahauri wasanii wenzangu kuendeleza na kudumisha amani ili Rais wetu aweze kufanya yale aliyotuahidi,” alifafanua.

Akiuzungumzia ushindi huo, mchezaji na kocha wa zamani wa Zanzibar Heroes, Salum Bausi Nassor, alimpongeza ushindi huo, alisema imani yake kwa kiongozi huyo atatekeleza ahadi alizozitoa kwa wananamichezo ikiwemo ya kuimarisha michezo kwa kutafuta udhamini.

“Nina furaha kubwa sana kwa ushindi wa Rais wetu huyu mteule naamini sekta ya michezo itanawirika na kama alivyozema ligi kuu ya Zanzibar atajitahidi kuitafutia mdhamini imani yangu kwake hilo halitomshinda,” alisema Bausi.