HANIFA SALIM MOHD
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imewanasihi wananchi kuendelea kuilinda amani iliyopo ndani ya nchi huku wakiingia katika uchaguzi tarehe 28 kwa salama na amani sambamba na kujiepusha kukaa makundi baada ya kupiga kura.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, aliyasema hayo katika mkutano wa wazazi na walezi wa Micheweni Pemba, kufuatia tukio la uvunjifu wa amani lililojitokeza hivi karibuni uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

“Jambo lililofanyika limewatia dosari watu wa Pemba, nawanasihi wazee wangu matendo ya uvunjifu wa amani yasije yakajirudia tena endapo mtu atakua anamtuhumu mwenziwe kwa kumfanyia ambavyo hapendi upo utaratibu wa kisheria na sio kuchukua hatua mikononi mwake,” alisema.

Alieleza kufuatia tukio la uvunjifu wa amani ambalo limefanywa kila aliehusika na tendo hilo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kwa namna moja ama nyengine na kuwataka wananchi washirikiane na wasameheane kwa yaliyojitokeza.

“Wapo watakaopiga kura ya mapema siku ya leo ni watu maalumu ambao ni vikosi vya ulinzi na usalama na watu wa tume wenyewe, ambao hawatopata fursa hii kwa ajili ya tarehe 28, kwani watakuwa na kazi moja tu yakutulinda na kutusimamia kupata haki yetu ya kupiga kura kwa salama
na Serikali imejipanga vizuri kuhusu suala la ulinzi” alisema.