ZIMEBAKIA wiki zisizozidi tatu kwa wananchi wa Zanzibar na watanzania kwa ujumla kwenda kukamilisha haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa viongozi wapya wa kisiasa watakaodumu madarakani kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Tunaipongeza sana Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kazi kubwa iliyoifanya na inayoendeleza kuifanya ya kuhakikisha inaweza mazingira mazuri ya maandalizi ya uchaguzi huo.

Tunazielewa jitihada zote zinazochukuliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, lengo lake ni kuhakikisha zoezi hilo linahitimika kwa nchi kubakia na kudumu kwenye amani tuliyonayo.

Tume hiyo kwa kushirikiana na vyama vya siasa hapa Zanzibar waliandaa, kukubaliana na hatimaye kusaini muongo wa maadili ya uchaguzi, muongozo ambao unaelezea kipi kinapaswa kufanywa na vyama vya siasa na wagombea wao.

Kwa hakika muongozo huo wa maadili hauna mwanya wa kukipendelea chama chochote, ndio maana vyama vyote vilihusika kuusaini baada ya kukubaliana nao.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa muongozo huo wa maadili ya uchaguzi, wapo baadhi ya wapambe wa vyama vya siasa na wagombea wameanza zoezi haramu kutaka kuuharibu uchaguzi wetu.

Kwa mujibu wa taarifa, wapo baadhi ya viongozi waandamizi wa vyama vya siasa katika maeneo mbalimbali wanapita nyumba kwa nyumba huko mitaani sio kwa ajili ya kuomba kura, bali kwa kununua shahada za kupigia kura.

Hapa tunaomba tueleweke vizuri, hatuwasemi wale wanaopita nyumba kwa nyumba kupiga kampeni za kuomba kura kwa wagombea wao, tunaowasema ni wale wanaowashawishi wananchi wawauzie shahada zao za kupiga kura jambo ambali ni kinyume cha sheria.

Zoezi hilo la ununuzi wa shahada za kupigia kura linaendelea katika mitaa mbalimbali ambapo wapambe wa chama kwa niaba ya kiongozi mkubwa wa chama wanagonga milango kununua shahada hizo kwa wananchi.

Mbinu zao ni kwamba wanapita katika nyumba ambayo wanauhakika haina wafusi wao na huingia kwa lengo la kumpigia kampeni mgombea wao, mwishowe huonesha fedha ili wauziwe shahada.