NA HAFSA GOLO

WAKATI leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuhutubia wanaCCM na wakaazi wa mikoa mitatu ya Unguja, wananchi wameeleza kuridhishwa na kazi anayoifanya toka aingie madarakani 2015.

Wakizungumza na gazeti hili wamemuelezea kiongozi huyo kama ni mkombozi wa wanyonge ambae ameonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kwamba wanaamini ataisaidia Zanzibar katika mabadiliko ya kiuchumi.

Walieleza kama ilivyokuwa katika maeneo mengine, ziara yake licha ya kuwa ya muda mfupi, itasaidia kuongeza matumaini mapya ya kimaendeleo kupitia mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.

Mmoja ya wananchi hao, Zahoro Ali Zahoro (63) alisema kutokana na uwezo na uadilifu wa utekelezaji wa majukumu ya kazi Watanzania wengi wanaendelea kumthamini sambamba na kujenga matumaini kuingia katika mageuzi katika mahitaji ya wananchi.

“Wengi tunatarajia Zanzibar itapiga hatua kubwa ya maendeleo, sambamba na kuwa na mafanikio kama nchi nyengine za visiwa kufuatia na mashirikiano ya kikazi kati ya viongozi hao wa pande mbili hizo,” alisema.

Naye Zaituni Faraji Idarous (47) alisema pamoja na kwamba Dk. Magufuli amekuja kwa ajili ya kampeni za chama cha mapinduzi (CCM), anaamini Wazanzibari wengi watapata nafasi ya kumsikiliza kiongozi huyo mtetezi wa wanyonge bila ya kujali itikadi zao za siasa, dini, rangi wala kabila.

Kwa upande wake Ali Hamadi Yussuf (39) aliyejitambulisha kama mwanachama wa chama cha ACT – Wazalendo aliwaomba wananchi wa zanzibar kuwa na matuaini kwa kiongozi huyo.

“Tuacheni utashi wa kisiasa Dk. Magufuli ni kiongozi wa watu wote, lililobaki ni ushabiki tu wa kisiasa lakini panapo ukweli uongo hujitenga,” alieleza kijana huyo.

Naye Said Juma Fikirini (45), alisema ipo haja kwa serikali kupitia CCM kuandaa ratiba nyengine kwa kiongozi huyo ili aweze kuwafikia wananchi wa Zanzibar katika mikoa yote kwani watu wanahitaji kusiliza mipango na mikakati yake ya maendeleo hasa kwa visiwa vya Zanzibar.