UFALME wa Eswatini unaendelea kuchukua jitihada za kuhakikisha unaimarisha haki za wanawake hasa wale waliomo kwenye ndoa.

Taifa hilo limeanzisha sheria ya kuwafungulia mashitaka waume wanaowabaka wake zao, hatua iliyowakasirisha wanaume wengi kwenye jamii ya Swatini ambayo inafuata misingi ya kihafidhina.

Siku chache zilizopita mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 34, aliyefahamika kwa jina la Nhlanhla Dlamini alikuwa mtu wa kwanza kushitakiwa chini ya sheria mpya inayokataka mume kumbaka mkewe.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo Nhlanhla Dlamini, alifikishwa mbele ya mahakama nchini humo akikabiliwa na shitaka la kulazimisha tendo la ndoa kwa mkewe ambapo kwa mujibu wa sheria mpya nchini humo kufanya hivyo kubachukulia kama ubakaji.

Kwa kutumia sheria ya makosa ya kijinsia na vurugu za nyumbani (SODV) ya mwaka 2018, ambayo inakataza tendo la ndoa kati ya mume na mke bila ya kupatikana idhini.

Kutokana na Nhlanhla Dlamini kulazimisha na kutumia nguvu kufanya tendo la ndoa kwa mkewe polisi nchini humo walimtia mbaroni na kumshitaki kwa kosa la ubakaji.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 14 mwaka huu, ambapo jalada kesi hiyo lilifikishwa mahakama kuu iliyopo mjini Mbabane, hata hivyo aliachiliwa kwa dhamana ya dola 3,400.

“Ni kesi ya kwanza kuripotiwa na kusikilizwa mbele ya mahakama ya wazi”, msemaji wa kikundi cha Swaziland cha hatua dhidi ya dhuluma (SWAGAA) Slindelo Nkosi aliliambia shirika la habari la AFP.

Kwa mujibu wa sheria hiyo iliyopitishwa mwaka jana wanaobainika kufanya makosa hayo wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela, wakati wahalifu waliorudia kosa hilo wanaweza kufungwa hadi miaka 30.

Kesi hiyo ya kihistoria ilishangaza watu wengi nchini humo. Taifa hilo pekee la kifalme barani Afrika, lililokuwa likijulikana kama Swaziland, linatajwa kuwa na utamaduni uliozoeleka wa mfumo dume.

Kiongozi wake, Mfalme Mswati III, ana miliki wake 14 tangu alipovishwa taji la ufalme mnamo mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 18, akiwa na watoto wanaozidi 25.

Mfalme Mswati III anachukuliwa kama mtawala anayependa maisha ya anasa na starehe, huku asilimia 63 ya raia wa nchi hiyo milioni 1.3 wa nchi yake wakiwa wanaishi katika hali ya umaskini.

“Sheria hii ni kinyume na maadili ya utamaduni wetu wa asili kama waswazi,” alisema mfanyabiashara Sabelo Mahlangu akizungumza na shirika la habari la AFP.

“Huwezi kuniambia kwamba mke niliyemuoa kwa kumlipia mahari, kulingana na mila na desturi zetu, anaweza kusema mume wake amembaka, hichi ni kichekesho kikubwa”, alisema mfanyabishara huyo.

“Upuuzi gani huo?” anauliza. “Hata biblia inaonya dhidi ya wanandoa kunyimana haki yao ya tendo la ndoa.”

Mitazamo hiyo ya Mahlangu inaungwa mkono kote nchini humo, hata hivyo wanawake wengi wameifurahia vya kutosha sheria hiyo na kuhisi utasaidia matumizi ya nguvu dhidi ya wanaume wanaolazimisha tendo la ndoa.

Katika mtandao wa kijamii wa Facebook, Ndosi Shenge, aliwasisitiza wanaume kuwa na wanawake kadhaa “ili mmoja anapokuwa hataki kufanya tendo la ndoa, mwanamme aweze kwenda kwa mpenzi wake mwengine”.

Lakini kwa mjane na mama wa watoto wawili, Sizakele Langa, sheria ya SODV ni muhimu katika kuwalinda wanawake walio kwenye ndoa kwavile kwa miaka mingi wanaume wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake bila ya kuwajibishwa kwa namna yoyote ile”.

Langa alisema alikuwa kwenye ndoa ya miaka 12, baada ya kuchoka kubakwa na aliyekuwa mume wake.

“Alikuwa na kawaida ya kutaka kufanya tendo la ndoa kwa lazima kila baada ya ugomvi kati yetu. Ninapomkatalia hunikamata kwa nguvu,” aliliambia shirika la habari la AFP.

Aliongeza kwamba alikuwa akizidiwa nguvu na mumewe, naye hakutaka kupiga kelele kwa kuhofia kuwaamsha watoto wake wanaokuwa wamelala ili kuepusha wasijue kile kinachoendelea katika maisha yake na baba yao.

“Familia yangu isingeniamini kwamba mume wangu akinibaka, hata polisi pia wasingeniamini.”

Unyanyasaji wa kijinsia ni kitu cha kawaida katika taifa hilo lilozungukwa na mataifa mengine ikiwa ni pamoja Msumbiji pamoja na Afrika Kusini. Lakini ni nadra kwa wahalifu wa tendo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kulingana na takwimu za polisi za mwaka 2019, katika kipindi cha miezi saba Eswatini ilirikodi vitendo 2,900 vinavyoangukia kwenye sheria hiyo ya SODV.

Mkurugenzi wa kikundi cha watafiti cha Wanawake na Sheria nchini Afrika Kusini, Colane Hlatshwayo, alisema ni inashtusha kuona kwamba jamii inaliangalia kosa la ubakaji wa wanawake kama kitu cha kawaida kwa sababu tu wanawake hao wamo ndani ya ndoa.

Changamoto ni kwamba “mmoja wao ana nguvu zaidi ndani ya ndoa na anaamini hahitaji idhini ya mwenziwe kufanya tendo la ndoa,” alisema Hlatshwayo.

Nkosi wa kikundi cha SWAGAA alilieleza tatizo hilo la ubakaji wa ndani ya ndoa kuwa linasababisha mabishano makubwa kwavile watu wengi bado hawajalielewa vizuri.

“Kuna hisia mbaya ya umiliki inayoongezeka miongoni asilimia fulani ya wanaume, haswa baada ya kuhalalisha uhusiano wake na mwanamke baada ya kuilipa familia yake mahari.

“Mtazamo huu umechangia kuongezeka kwa manyanyaso ndani ya ndoa kwa sababu mmoja wao anaamini anamliki mwenziwe”, alisema Nkosi.