TUCHUKUE fursa hii kwa dhati kabisa kuwapongeza sana wananchi wa Zanzibar, kwa kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kitaifa la upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Zoezi la uchaguzi mkuu lililowashirikisha wananchi wenye sifa za kupiga kura hapa nchini, ni utekelezaji wa misingi ya kidemokrasia inayotoa fursa kwa wananchi kuwachagua viongozi wao wanaowapenda na watakaoshirikiana nao katika maendeleo.

Sote kabisa kila mmoja wetu anapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kulimaliza zoezi hilo kwa amani na utulivu mkubwa.

Tunaelewa zilikuwepo changamoto ndogo katika baadhi ya maeneo kwa hasa kwenye zoezi la upigaji wa kura ya awali iliyofanyika Oktoba 27 mwaka huu lililowashirikisha watu wa makundi maalum.

Tuvipongeze sana vikosi vya ulinzi kwa kudhibiti usalama uliofanikisha kwenye zoezi la upigaji wa kura ya mapema, ambapo hali hiyo iliwezesha wananchi kupiga kura kwa amani kwenye zoezi la Oktoba 28.

Kiukweli tunashangaa sana, huku tukijiuliza kwanini kutokee vurugu? Kwanini watu wasababishe ghasia kwneye zoezi la upigaji kura zoezi la kura ya awali ambapo msingi wake upo kisheria.

kura ya awali

Lakini suala la upigaji kura ya awali mbona limeelezwa na kufafanuliwa vyema kanuni za uchaguzi ambapo baadhi ya vyama walisaini na kukubaliana na uwepo wa kura hiyo.

Suala la kuipinga kura ya mapema halikupaswa kusababisha vurugu na kama wakuu wa vyama wanaopinga wako makini walipaswa kupiga suala hilo kwa kutumia sheria.

Kwa sababu kura mapema ni suala la kisheria, walipaswa wale wanaolipinga walifikishe mahakamani, kwani chombo hicho ndicho chenye mamlaka kisheria kutafsri sheria na uhalali wake.

Inashangaza sana kuona baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kulichukulia  suala la upigaji wa kura ya mapema kama vile limechomekwa kinyemela na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Mawazo ya viongozi hao ni kwamba zoezi hilo la kura ya mapema ni kwa ajili ya kuvibeba ama kuvisaidia baadhi ya vyama vya siasa ili vishinde uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, tunavyoamini viongozi wa vyama vya siasa wanaopinga uwepo wa kura ya mapema waangalie upya mtazamo wa kulipinga na kamwe wasisababishe vurugu kwa vitendo na kauli zao.