NEW YORK,MAREKANI

WIZARA ya Mambo ya Nje ya Marekani imeidhinisha ombi la Japani la kuwarejesha nchini humo wanaume wawili waliokamatwa kwa madai ya kumsaidia aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni ya magari ya Nissan Motor Carlos Ghosn kutorokea Lebanon.

Waraka wa mahakama unaonesha kuwa Wizara hiyo ilitoa idhini ya Michael Taylor na mwanawe wa kiume Peter Taylor kurejeshwa nchini Japani wiki hii. Wote hao ni wakaazi wa Massachusetts.

Wawili hao walitarajiwa kusafirishwa kwenye ndege ya kuelekea nchini Japani. Lakini jaji aliridhia ombi la mawakili wao la kusitisha kuwarejesha Japani.

Japani iliwasilisha ombi la kutaka warejeshwe nchini humo kwa misingi ya mkataba wa urejeshaji wa pande mbili baada ya wanaume hao kukamatwa na wapelelezi wa Marekani mwezi Mei.

Mahakama moja kuu ya Marekani iliridhia kurejeshwa kwao nchini Japani mwezi Septemba mwaka huu.