NA MWAJUMA JUMA

MKURUGENZI wa Elimu ya Sekondari Asya Iddi amesema kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wanawake, hasa wa vijijini juu ya kushiriki mchezo wa mpira wa miguu pamoja na kuwaendeleza.

Mkurugenzi huyo aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya uongozi ndani ya mpira wa miguu kwa wanawake yaliyofanyika Amaan hivi karibuni.

Alisema  wanawake ambao wamepata mafunzo ni wajibu wao sasa kujitoa na kufika vijijini, kulielezea hilo ili wawe mabalozi wazuri kwa soka la wanawake.

Alifahamisha kwamba yeye binafsi amefarijika sana kuona wanawake wamejitoa kusoma uongozi wa mpira wa miguu, ambao kwa kiasi kikubwa watasaidia kusukuma mbele gurudumu la mchezo huo hapa Zanzibar.

“Nimefarijika sana kuwaona wanawake wanasomea mpira wa miguu, kwani nilihangaika sana katika uongozi wangu kuhakikisha somo la ‘Physical Education’ linakuwa moja katika mitaala inayosomeshwa ili kuwajenga watoto mapema kimichezo”,alisema.

Hivyo alisema hatua hii ambayo imeoneshwa na Shirikisho la Soka Zanzibar na lile la Tanzania TFF, ni nzuri na inalenga kuinua soka la wanawake ambalo linaonekana kudorora.“Wakishapata wao elimu ndio watakaoweza kusaidia kuelimisha juu ya suala hili”, alisema.