NA MARYAM SALUM

WANAWAKE Kisiwani Pemba, wametakiwa kuwa wakakamavu kwa kutoogopa changamoto zinazowakabili katika kugombea nafasi mbali mbali za Uongozi na badala yake wazitumie kama silaha ya kufikia mafanikio yao.

Hayo yalielezwa na wajumbe wa kamati  ya wanaume mawakala wa mabadiliko Kisiwani humu, katika ukumbi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania -TAMWA Zanzibar, wakati  walipokuwa kwenye mkutano wa siku moja kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu yao.

Walisema kuwa lengo la kamati hizo ni kuhakikisha wanapita kila eneo ndani ya jamii kukutana na watu mbalimbali kuelimisha na kushawishi kuhusu umuhimu na nafasi ya wanawake katika kugombea nafasi za uongozi kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi.

Yusuf Abdalla Ramadhani, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alisema kuwa lengo la TAMWA kuunda kamati hizo ni kuhakikisha wanaifikia jamii kwenye maeneo  yao kuwapatia elimu  ambayo itakuwa chachu ya kuwabadilisha wanawake katika kugombea nafasi za Uongozi kwa maslahi ya jamii.

Alisema kuwa kutokana na elimu wanayoitoa kwa wananchi hasa kwa wanawake, vijana wengi kwa katika kipindi cha mwaka huu wameweza kujitokeza katika majimbo yao kujaza fomu za Uongozi na wapo ambao

wamebahatika kupata nafasi hizo.

Mwalimu Amour Rashid Ali, alisema kuwa malengo ya TAMWA kuunda makundi hayo ni kuona kwamba wanawake wanakuwa na mabadiliko katika kujitokeza kwenye nafasi za Uongozi kwa maslahi ya jamii.

Alifahamisha kuwa TAMWA imefanikiwa kwa asilimia kubwa katika kuwakomboa wanawake kiuchumi, kwani wamekuwa wakiwapatia miradi mbali mbali na nyenzo tofauti za kuhakikisha wanajikomboa kiuchumi na

kuondokana na Umasikini.

Nae Mratibu wa TAMWA Ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said amezitaka, kamati hizo kuendelea kuelimisha jamii ili kuhakikisha kwamba lengo la upatikanaji wa mabadiliko yanakuwepo kwa wanawake.

Mkutano huo ulijumuisha  makundi mbali mbali ya kijamii likiwemo kundi la Viongozi wa dini, pamoja na Viongozi wa vyama mbali mbali vya Siasa Kisiwani humu.