ABUJA,NIGERIA

MCHAKATO wa kuchagua kiongozi ajaye wa Shirika la Biashara Duniani-WTO umeingia katika hatua ya mwisho ambapo wanaowania nafasi hiyo wamechujwa kutoka wagombea watano hadi wawili.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la WTO alitangaza kuwa wagombea wawili wa nafasi ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo ni aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala na Waziri wa Biashara wa Korea Kusini Yoo Myung-hee.

Wagombea hao wawili ni wanawake, ikiashiria kuwa WTO itakuwa na kiongozi mkuu mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia yake.

WTO inapanga kufanya mashauriano zaidi na itamchagua kiongozi wake mpya mapema mwezi ujao.

Shirika hilo lenye nchi wanachama 164 limesema kuwa linalenga kuhakikisha mtiririko mzuri wa biashara, unaoweza kutabiriwa na ulio huru kadri iwezekanavyo.

Lakini shirika hilo linakabiliwa na shinikizo la kufanya mabadiliko ya ndani.Wachambuzi wanasema shirika hilo halijajizatiti ipasavyo kukabiliana na masuala mbalimbali huku kukiwa na ongezeko la mizozo ya kibiashara, kama ule wa kati ya Marekani na China.