PARIS, UFARANSA

Rais Emmanuel Macron

WATU wanne, akiwemo mtoto mdogo, wametiwa nguvuni nchini Ufaransa, kufuatia kuuawa kwa kukatwa kichwa, mwalimu mmoja nje ya skuli yake, tukio ambalo rais Emmanuel Macron, ameliita la kigaidi.

Muuaji, ambaye jina lake halijatajwa, alipigwa risasi na polisi, walipokuwa wakijaribu kumkamata na baadaye alikufa kutokana na majeraha.

Watu wote wanne waliokamatwa ni ndugu wa muuaji huyo, ambapo tukio hilo lilitokea kwenye maeneo ya mji mkuu, Paris, karibu na skuli anayofundisha mwalimu huyo.

Ripoti zinaeleza kwamba, mwalimu huyo wa somo la historia, alikuwa amewaonesha wanafunzi wake picha, zenye katuni za kumdhihaki Mtume Muhammad (SAW).

Hata hivyo, mzazi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, kabla ya kuonesha katuni hizo, mwalimu huyo alikuwa amewaomba wanafunzi wa Kiislamu watoke nje ya darasa, kwani hakutaka kuwaumiza hisia zao.