NA HAFSA GOLO
MFUKO wa kunusuru kaya masikini shehia ya Jang’ombe Urusi, umetoa elimu kwa walegwa 95 wanaoishi katika kaya hiyo kutumia vyema fedha za miradi zitakazo tolewa na mfuko huo, ili wafikie malengo ya kujikwamua na umasikini.
Msimazi wa kaya masikini, Nuru Abdallah Mwalimu, alitoa wito huo katika kikao maalumu cha kutathmini na kujadili miradi inayotekelezwa na kaya hiyo, mkutano uliofanyika katika tawi la CCM Jang’ombe.
Alisema fedha za kuendeshea miradi kwa kaya masikini ndani ya shehia hiyo zinatarajiwa kutolewa hivi karibuni , hivyo ni vyema kuhakikisha kunakua na utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha hizo, ili uweze kuleta tija na kutimiza azma ya Serikali katika kuondosha changamoto za kimaisha.
“Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanga mikakati mingi kuhakikisha inaanzisha miradi ya kaya masikini, ili kuwakomboa wananchi wake” alisema.
Aidha alisema iwapo kina mama hao watafuata maelekezo na taaluma ya uendeshaji wa biashara wanayopatiwa itasaidia kupanua wigo na ustawi mzuri wa maisha.
Nae Sheha wa shehia ya Jang’ombe Urusi, Yussuf Haji Mtumwa, alitaja miongoni mwa miradi itakayotekelezwa katika shehia hiyo ni pamoja na ufugaji wa kuku, mafuta na sabuni.
Aidha alisema atahakikisha anasimamia vyema jukumu hilo, ili watu hao waweze kufaidika sambamba na kuondokana na umasikini.
Mbali na hilo alihimiza suala la umoja na mshikamano katika uendeshaji wa miradi hio, kwani ni miongoni mwa njia sahihi za kutimiza ndoto zao.