Wampongeza kwa mazuri aliyowafanyia

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein juzi usiku alikuwa mgeni rasmi katika taarab maalum iliyoandaliwa na vikundi mbali mbali vya Taarab vya hapa Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.

Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar, ambapo viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali, wasanii pamoja na wananchi kadhaa walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.

Mapema wasanii hao wakisoma risala yao ya shukurani kwa Rais Dk. Shein, walimpongeza kwa kusimamia na kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka 10, huku akisimamia amani na utulivu sambamba na kuwajali wananchi wake wakiwemo wasanii.

Wasanii hao walieleza kuwa Rais Dk. Shein amefanya mambo mengi muhimu na mazuri katika kipindi chake cha uongozi akiwa Rais wa Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuunda Wizara maalum ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambayo iliwawezesha  wasanii kukaa pamoja kwa  kufanya kazi na kujadiliana mambo mbali mbali ya uchumi na maendeleo.

Jengine waliolieleza wasanii hao ni pamoja na kuwatengenezea studio ya kisasa ya kurikodi filamu na muziki, huko Rahaleo Jijini Zanzibar, studio ambayo imewawezesha kufanya kazi zao kwa ustadi mkubwa.

Wasanii hao walieleza kuwa Rais Dk. Shein ameweza kukiimarisha Kikundi cha Taifa cha Taarab kwa kukipa vifaa vipya na ofisi ya kufanyia kazi, pamoja kurejesha maonyesho ya fensi ambayo yamewapa wigo mpana wasanii na kuwa wabunifu wa kazi mbali mbali za kisanii.

Aidha, wasanii hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuziunganisha Sheria za Baraza la Sanaa na Bodi ya Sensa na Filamu pamoja na kuwaangalia wasanii wagongwe na wagonjwa kwa kutembelewa na kuweza kusaidiwa.

Sambamba na hayo, wasanii hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwasaidia fedha maalum waasanii wote waliofika katika hafla hiyo, huku wasanii wao wakionesha furaha yao kwa kumpa zawadi maalum Rais Dk. Shein kutokana na uongozi wake bora na uliotukuka.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Omar Hassan ‘King’, akimkaribisha Rais Dk. Shein katika hafla hiyo alisema  Taarab hiyo imeandaliwa na wasanii wa Taarabu kutoka vikundi tisa, kikiwemo kikundi cha Taifa pamoja na vile vinavyojitegemea wakiwa na lengo la kumpongeza na kumuaga Rais wao.