TOKYO,JAPANI

WASIMAMIZI  wa masuala ya kifedha wa Japani watafanya ukaguzi kwenye ofisi za Soko la hisa la Tokyo, TSE kuhusiana na usitishwaji wa shughuli za soko hilo kwa siku nzima uliotokea mapema mwezi huu.

Uamuzi huo wa Shirika la huduma za fedha kufanya ukaguzi huo, ulikuja baada ya kupokea ripoti kutoka TSE inayoelezea chanzo cha usitishwaji huo na kuelezea hatua za kuzuia kutokea tena kwa tukio kama hilo.

Usitishwaji wa shughuli za soko hilo uliotokea Oktoba Mosi ulitokana na hitilafu ya vifaa na vifaa vya usaidizi kushindwa kufanya kazi.

Maofisa wa TSE walisema kasoro katika mfumo wa kompyuta na vitabu vya miongozo ulichangia tatizo hilo.

Maofisa wa shirika hilo walisema watahitaji kukagua jengo la ofisi hiyo ili kuangalia usimamizi wa ndani wa mfumo huo.

Maofisa hao wanalichukulia jambo hilo kwa umakini mkubwa kwani ni mara ya kwanza kutokea usitishwaji kama huo tangu mfumo wa uuzaji na ununuaji wa hisa ulipoanza kuendeshwa kwa kompyuta mwaka 1999.

Wanapanga kufikiria faini za kuitoza TSE ikiwemo amri ya uboreshaji wa biashara.