NA HUSNA SHEHA

WASIMAMIZI wa uchaguzi katika vituo vya kupigia kura wametakiwa kuacha ushawishi wakati wanapoendelea na zoezi hilo ndani ya majimbo yao.

Wakizungumza na wasimamizi wa vituo vya kupigia kura wa tume ya Taifa NEC kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuandaa watendaji hao na zoezi hilo wasimamizi wa majimbo matano ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini wamewataka watendaji hao kuacha ushawishi wakati zoezi litakapoendelea.

Wakuu hao walisema tume ya Taifa NEC inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuandaa zoezi hilo ili kuwapa nafasi wananchi kuchagua wagombea watakaoweza kuleta mabadiliko katika nchi pamoja na kutimiza haki  yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wao watakaowaridhia.

Wasimamizi wa tume ya uchaguzi  Taifa NEC Iliyasa Pakacha Haji alisema wajibu wa wakuu wa vituo kuhakikisha zoezi na mchakato mzima wa uchaguzi linakwenda vizuri bila ya kusababisha zoezi hilo kuharibika na kupelekea kufutwa kwa uchaguzi.

Alieleza kuwa wasimamizi watakapofanya kazi kwa kufuata matakwa yao wanaweza kupelekea nchi kuingia kwenye machafuko endapo hawatozingatia majukumu yao na kupelekea nchi kukosa amani iliyopo.

Hivyo aliwatahadharisha watendaji hao kufanya kazi kwa uzalendo,mashirikiano na upendo kwenye kipindi hicho ili kutimiza wajibu wa kati yao kwa mujibu wa maelekezo ya tume.

Nao wasimamizi wa zoezi hilo waliomba kupatiwa utaratibu maalum wa kupiga kura pale watakapopangiwa mbali na vituo vyao ili washiriki zoezi la kupiga kura kwani kinyume na hivyo watakosa haki yao ya kupiga kura.

Watendaji waliopatiwa mafunzo ni kutoka majimbo ya Tumbatu, Chaani, Nungwi, Kijini na Matemwe.