NA HUSNA SHEHA

WATU wasiojulikana wamepaka kinyesi madarasa mawili ya skuli ya msingi ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo, Shaaban Sarboko Makarani, alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi.

Alieleza tukio hilo limetokea baada ya walinzi wa skuli hiyo kutowajibika ipaswavyo kwani hadi wanaondoka kazini hawajafika katika eneo la skuli.

“Mimi na Mwalimu wa Msaidizi tulikuwepo hapa jana (Juzi) mpaka usiku wa saa 2:00, lakini hajatokea mlinzi hata mmoja na bendera pia haijapachuliwa tumefika kuondoka,”alisema.

Aidha alisema kufanyiwa kitendo hicho sio mara ya kwanza imekuwa ni wazowefu wa kuwafanyia lakini bado na hatujawagundua wahusika wa hujuma hizi,”ni mwezi wa pili huu tena wanatufanyia hivyo lakini bado hatujawajua,”alisema.

Hata hivyo, anaeleza kwamba anawasiwasi wa kushirikishwa wanafunzi wa skuli hiyo kutokana na hali ya mazingira inavyo kwenda.

Vile vile alisema vitendo hivyo vilizidi wakati zilipofungwa skuli kwa maradhi ya corona, hali ambayo ni hatarishi kwa afya za wanafunzi wanaosoma hapo.

“Katika kipindi cha maradhi ya corona skuli waligeuza ni vyoo kila tukija tunakuta wamepaka kinyesi,”alisema.

“Suala hilo linafanywa sio kwa uhaba wa vyoo katika nyumba za  wananchi isipokuwa kuna baadhi ya watu maalumu wanafanya hayo,”alisema.

Alieleza kwamba mbali ya  hujuma hizo pia vimeharibiwa vyoo ambavyo vilijengwa na serikali kupitia mradi wa vyoo, ambapo jumla ya vyoo 16 vikiwemo viwili vya walemavu vilifanyiwa hujuma ya kuvunjwa kwa kung’olewa milango na paipu pamoja na kung’olewa masinki na milango ya makaro na kufikia hali ya kutoweza kutumika.

Vile vile alisema kwamba mbali ya kutia kinyesi pia kunaharibiwa mazao ya skuli hiyo, hali ambayo inarudisha nyuma kimaendeleo ya skuli hiyo.